Rapa King Kaka afichua kwanini anaamini kuna uchawi

Rapa huyo aliamini kuna uchawi baada ya kukutana nao baadaye maishani.

Muhtasari

•Bosi huyo wa Kaka Empire alifunguka jinsi siku za nyuma aliwahi kushuhudia uchawi kwa njia isiyo ya moja kwa moja.

•"Sijui kilichofanyika. Lakini najua kilichofanyika kilifanyika na niko hapa sasa," King Kaka alijibu.

Image: INSTAGRAM// KING KAKA

Mwimbaji wa nyimbo za kufoka Kennedy Ombima almaarufu King Kaka amedokeza kwamba anaamini kweli uchawi upo.

Akizungumza katika mahojiano na mwanavlogu Oga Obinna, King Kaka hata hivyo alisema kuwa hapo mwanzoni hakuamini kuwa kuna uchawi na alifanya hivyo baada ya kukutana nao ana kwa ana baadaye maishani.

Bosi huyo wa Kaka Empire alifunguka jinsi siku za nyuma aliwahi kushuhudia uchawi kwa njia isiyo ya moja kwa moja.

"Kitambo, miaka kama saba kumi hivi, kuna mtu nilikuwa najua alirogwa. Alikuwa karibu sana akarogwa," Kaka alisimulia.

Aliongeza, "Sikuwa naamini kuna uchawi. Alafu mtu ambaye nilikuwa najua akaanza kufanya vitu vya ajabu na si kuchizi!"

Alifichua kuwa mtu huyo wa karibu ambaye alifanyiwa uchawi alianza kuzungumza na watu wasiokuwepo wakiwemo waliofariki.

King Kaka alikuwa akijibu swali kama anaamini kuwa nguvu za giza ndizo zilizosababisha ugonjwa wa ajabu uliomkumba mwaka 2021.

"Sijui kilichofanyika. Lakini najua kilichofanyika kilifanyika na niko hapa sasa," alijibu.

Rapa huyo alibainisha kuwa Mungu alihusika katika uponyaji wake wa kimuujiza huku akieleza kwamba amekuwa naye daima.

"Mimi huwa naamka na kitu cha kwanza ni kumwambia Mungu asante, kila asubuhi," alisema.

Kaka alisema uponyaji wake ulikuwa wa ajabu kwani wahudumu wa afya katika hospitali aliyokuwa amelazwa walithibitisha kuwa si watu wengi wanaotoka humo wakiwa hai baada ya kulazwa katika hali mbaya kama yeye.

King Kaka alifichua kwamba mchakato wa uponyaji wake ulianza usiku mmoja wakati bado akiwa amelazwa katika hospitali ambapo alianza kuona mambo yasiyo ya kawaida mwendo wa saa tisa usiku.

"Nilianza kuona vitu sijui. Nilianza kuona mwangaza, nikaona giza. Niliona ni wakati wangu wa kuishia. Niliambia Mungu kama wakati wangu niko tayari. Huwa inafika mahali hata unakubali kifo," alisimulia.

Alisema baada ya kufichuliwa mambo ya ajabu alimuomba Mungu na kufanya amani naye kwani alihisi anakaribia kufa.

Kiajabu, asubuhi iliyofuata alipata kifungua kinywa kwa mara ya kwanza baada ya siku tano hivi. Pia alikunywa supu baadaye.

"Hivyo ndivyo nilianza kula. Baada ya siku tatu, nne hivi nilikuwa natembea huko hospitali," alisema

Aliruhusiwa kuenda nyumbani siku tano baada kupata ufunuo wa ajabu usiku.

King Kaka alifichua kwamba uhusiano wake na Mungu umekuwa mzuri kwa miaka mingi ya maisha yake.