Rayvanny afichua kiasi kikubwa cha pesa alicholazimika kumlipa Diamond ili kuondoka Wasafi

Rayvanny alidai alilipa Ksh 68.9m ili kutamatisha kandarasi yake na WCB.

Muhtasari

•Rayvanny alifichua Jumatatu wakati akikabiliana na mwimbaji mwenzake Harmonize kwa vita vya maneno kwenye mtandao wa Instagram.

•Harmonize  alikosoa madai ya Rayvanny huku akidai kuwa mwimbaji huyo mwenzake hajawahi kushika bilioni ya Tanzania. 

Rayvanny na Diamond Platmnumz
Image: INSTAGRAM
 

Staa wa Bongo Raymond Mwakyusa almaarufu Rayvanny alilipa shilingi bilioni 1.3 za Tanzania (Ksh 68.9m) ili kutamatisha kandarasi yake na WCB.

Rayvanny alifichua Jumatatu wakati akikabiliana na mwimbaji mwenzake Harmonize kwa vita vya maneno kwenye mtandao wa Instagram.

Katika vita ya kuthibitisha nani mkubwa kuliko mwingine, bosi huyo wa lebo ya Next Level Music alimbainishia Harmonize kuwa yeye alilazimika kulipa zaidi ya mara dufu  ya kiasi alicholipa ili kukatisha mkataba wake na lebo ya Diamond.

"Ulilipa Wasafi 600M umelia kwenye media zote mzee, kama hujui mimi nililipa Wasafi bilioni 1.3. Ukihisi nimeongeza sufuri fuatilia au nenda BASATA ukaulize na umeona nimeongea wapi?" Rayvanny aliandika.

Aliongeza, "Pesa sio kitu kwangu, kikubwa heshima ndio kitu ninachokithamini.Ukiona siku nimenga ujue nimekosewa heshima kufika mwisho."

Rayvanny alijigamba kuwa viwango vyake ni vya juu zaidi ambavyo msanii huyo mwenzake wa zamani katika WCB hawezi kufikia.

Harmonize hata hivyo alikosoa madai ya Rayvanny huku akidai kuwa mwimbaji huyo mwenzake hajawahi kushika bilioni ya Tanzania. 

Pia alisisitiza kuwa Rayvanny bado amefungwa katika Wasafi na hajaweza kupata uhuru kamili wa kujisimamia mwenyewe.

"Mnataja taja hela baadae mnawalalamikia TRA kwenye hiyo bilioni unajua ni shingapi ya serikali 😂😂 Mmelipa? Bilioni utoe wapi mdogongu!!," alisema.

Harmonize alimtaka mwanamuziki huyo mwenzake kuonyesha barua ya kutamatishwa kwa kandarasi yake na Wasafi ili kuthibitisha madai yake.

"Njoo ukae chini na wahuni tukuelezee inakuaga vipii namjua Huyoo!!," 

Rayvanny aliondoka katika Wasafi mwaka jana baada ya kuwa chini ya usimamizi wa lebo hiyo kwa takriban miaka sita.

Wakati akitangaza kuondoka kwake, alishukuru uongozi mzima wa WCB  ukiongozwa na Diamond ambaye amekuwa mwandani wake kwa kipindi kirefu.

“Miaka 6 sasa tangu tumeanza kufanya kazi pamoja na hii timu yangu, familia yangu, WCB Wasafi. Upendo, umoja vimekuwa nguzo kubwa saba kama timu. Mengi nimejifunza lakini pia mengi tumefanikisha tukiwa pamoja.. Shukrani za dhati kwa familia yangu Wasafi lakini pia kwa ndugu yangu Diamond Platnumz kwa kunipa nafasi dunia ione kipaji change nilichobarikiwa na mwenyezi Mungu ili kufika hapa nilipofika, kusaidia familia yangu na kufanikisha mengi katika maisha yangu,” Alisema katika video aliyopakia Instagram.

Staa huyo aliripotiwa kuondoka kwenye lebo hiyo ya Diamond ili kuangazia na kukuza lebo yake ya Next Level Music .

Wakati huo, ripoti kutoka Bongo zilidokeza  kuwa hatua yake kuondoka WCB  ilimgharimu takriban Tsh 800 (Ksh 40.9).