"Sio safari rahisi!" Mtangazaji Catherine Kasavuli afunguka kuhusu vita vyake na Saratani

Hata hivyo ameeleza imani yake kuwa hatimaye ataibuka mshindi.

Muhtasari

•Kasavuli anaendelea kupokea matibabu maalum katika hospitali ya Kenyatta baada ya kugundulika na saratani ya shingo ya uzazi.

•Kasavuli alidokeza kuwa vita vyake na ugonjwa wa saratani havijakuwa rahisi

Image: INSTAGRAM// CATHERINE KASAVULI

Mtangazaji wa habari mkongwe Catherine Kasavuli ametoa taarifa kuhusu afya yake na safari yake ya matibabu.

Kasavuli ambaye anaendelea kupokea matibabu maalum katika hospitali ya Kenyatta baada ya kugundulika na saratani ya shingo ya uzazi (Cervical Cancer) amekiri kwamba mwezi mmoja ambao umepita haujakuwa rahisi kwake.

Mwanahabari huyo hata hivyo ametoa shukran za dhati kwa familia yake, marafiki, wafanyikazi wenzake, Catherine Kasavuli Foundation, madaktari, wanamitandao na watu asiowajua ambao wamekuwa wa msaada mkubwa kwake.

"Natamani ningejibu meseji zenu zote, naziona na nashukuru sana. Mungu awakumbuke," alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Aliongeza, "Kwa watu maalum ambao wamejitokeza kuchangia damu Mungu awabariki, azidishe roho zenu nzuri, atimize matakwa ya moyo wenu. Kwa wanaochangia bili yangu ya matibabu, ninawapenda sana na Mungu awabariki."

Kasavuli alidokeza kuwa vita vyake na ugonjwa wa saratani havijakuwa rahisi. Hata hivyo ameeleza imani yake kuwa hatimaye ataibuka mshindi. Pia amewatia moyo watu wengine wanaopambana na hali hiyo.

"Si safari rahisi lakini ninaamini katika uaminifu wa Mungu na mafanikio yake. Kwa mtu yeyote anayepigana vita sawa - nakupenda, tutashinda, maisha ni kitu kizuri na tutaishi kusimulia hadithi zetu," alisema.

Habari kuhusu kuugua kwa mtangazaji huyo wa KBC zilikuja kujulikana hadharani wiki jana ambapo ombi la damu lilitolewa kwa ajili yake. Taarifa fupi ilitolewa kuwa amelazwa katika KNH na watu wa kundi lolote la damu wakaombwa kujitolea.

"Wapendwa marafiki, wafanyakazi wenza na watu wenye nia njema. Mwenzetu mpendwa Catherine Kasavuli amelazwa katika Mrengo wa Kibinafsi wa KNH. Kwa wale wanaoweza, anahitaji kuwekwa damu mishipani haraka," taarifa iliyofikia Radio Jambo ilisoma.

Wakenya pia wameombwa kumkumbuka mtangazaji huyo katika maombi yao na pia kutoa msaada wa aina nyingine yoyote.

Kituo cha KBC Channel 1 pia kilifanya ombi la msaada wa damu kwa ajili Bi Kasavuli kupitia kurasa za mitandao ya kijamii.

Kasavuli ,60, alikuwa mtangazaji wa kwanza wa habari wa kike nchini Kenya na amewahi kufanya kazi katika vituo kadhaa maarufu vya televisheni vya hapa nchini vikiwemo  KBC, Citizen TV na KTN.