Staa wa dancehall wa Jamaica, Konshens kuzuru Kenya mwezi Disemba

Konshens ametangaza kuwa atapitia Kenya wakati wa tamasha lake lijalo nchini Uganda.

Muhtasari

•Konshens ambaye anatarajiwa kutumbuiza Uganda tarehe 17 Desemba alisema hawezi kutembelea nchi hiyo jirani na kukosa kupitia Kenya.

•Konshens alikiri kukubali jina la majazi ambalo alibandikwa na Wakenya kufuatia uhusiano na upendo wake mkubwa kwa taifa hili.

Konshens
Image: HISANI

Msanii maarufu wa Dancehall kutoka Jamaica Garfield Delano Spence almaarufu Konshens ametangaza kuwa atapitia Kenya wakati wa tamasha lake lijalo nchini Uganda.

Katika taarifa fupi ya siku ya Jumanne asubuhi, mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 38 ambaye anatarajiwa kutumbuiza nchini Uganda tarehe 17 Desemba alisema kuwa hawezi kutembelea nchi hiyo jirani na kukosa kupitia Kenya.

"Kwa taarifa yenu, hakuna jinsi ninavyokuja Uganda niipendayo na nikose kusimama Kenya niipendayo hata kama ni hisia za likizo," Konshens alisema kupitia akaunti yake ya Twitter.

Msanii huyo wa dancehall aliendelea kuwaomba Wakenya kumpendekeza maeneo mazuri ya kutembelea nchini.

Konshens ambaye anatambulika na kusherehekewa sana nchini Kenya si mgeni humu nchini, tayari amefanya ziara mara kadhaa katika miaka iliyopita.

Upendo mkubwa wa mwimbaji huyo wa Dancehall na Reggea kwa Kenya pia ni dhahiri shahiri na amethibitisha hilo kwa ziara zake kadhaa. Konshens ni mgeni wa mara kwa mara nchini Kenya na ziara yake ya mwisho ilikuwa Desemba 2021.

Wakenya wengi pia wanamshabikia Mjamaica huyo na hata kumfuatilia kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Mapema mwaka huu, mwanamuziki huyo mahiri wa Dancehall alikiri kukubali jina la majazi ambalo alibandikwa na Wakenya kufuatia uhusiano na upendo wake mkubwa kwa taifa hili.

Upendo mkubwa wa mwimbaji huyo kwa Kenya uliwafanya watumiaji wa mitandao ya kijamii wabunifu kumpa jina Konshens Otieno na Mkenya mmoja hata akamtengenezea kitambulisho cha Kenya.

Konshens kwenye remix yake na rapa Boutross Munene ya wimbo maarufu 'Anjella' alionekana kulikubali jina hilo kwa moyo mkunjufu.

"Brace  pan di wall and fling it up gimmi nuh,

Konshens AKA Otieno,

Play with the two ni++le like Piano," Konshens aliimba.

Kwenye kitambulisho alichotengenezewa na Mkenya mbunifu, msanii huyo mzaliwa wa Jamaika alisemekana kuzaliwa Kisumu, Kenya.

Mapema mwaka jana baada ya tamasha lake la kusisimua humu nchini Kenya, pia alionekana kukubali jina hilo alilopewa huku akiwaaga Wakenya. Wakati huo, aliahidi kurudi baada ya miaka michache.

"Upendo mkubwa Kenya, imekuwa ya kweli, muungano wetu una nguvu kuliko awali. Tutaonana tena baada ya miaka 3/4 Konshens Otieno," aliandika kwenye Twitter na kuambatanisha na emoji ya bendera ya Kenya.