"Tunakupenda mpenzi" Akothee amfariji aliyekuwa mumewe baada ya kupoteza babake

Muhtasari

•Akothee alimfariji Jared na kusema hangekubali kuacha baba huyo wa watoto wake watatu aomboleze pekee yake bila wao kuwepo.

•Akothee alimtambua marehemu kama baba mkwe wake na kumtaja kama mwanamume mwenye bidii kubwa.

Akothee na Jared Okello
Akothee na Jared Okello
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Siku ya Ijumaa Akothee alijumuika na wakwe wake kuomboleza na kumzika baba ya aliyekuwa mume wake Jared Okello Otieno.

Bw Evans Otieno Maduma ambaye ndiye babu halisi wa binti watatu wa mwanamuziki huyo alizikwa nyumbani kwake katika eneo la Kanga, kaunti ya Migori.

Akothee alimtambua marehemu kama baba mkwe wake na kumtaja kama mwanamume mwenye bidii kubwa.

"Mapema leo (Ijumaa) nikijiandaa kwenda kuomboleza na familia yangu ya kwanza kabisa baada ya nyumba ya mama yangu,  pamoja na watoto wangu. Leo Baba mkwe wangu Bw Evans Otieno Maduma atazikwa. Ni mtu aliyefanya kazi kwa bidii. R.I .P BABA," Akothee aliandika chini ya picha yake akiwa safari kuhudhuria mazishi.

Akothee aliandamana na binti wake wawili wa kwanza, Vesha Okello na Rue Baby kuhudhuria mazishi hayo. Alisema Fancy Makadia hangeweza kuwepo kwa kuwa alikuwa anafanya mtihani shuleni.

Alichukua fursa hiyo kumfariji Jared na kusema hangekubali kuacha baba huyo wa watoto wake watatu aomboleze pekee yake bila wao kuwepo.

"Inasikitisha sana rafiki yangu. Pole kwake baba vesha. Kupoteza kwako ni kupoteza kwetu.Singeruhusu upitie haya pekee yako, unajua tulipotoka," Alisema Akothee kupitia Instagram.

Mama huyo wa watoto watano alimtambua mpenzi huyo wake wa zamani kama rafiki wake mkubwa na kumhakikishia kuhusu upendo mkubwa alio nao kwake.

"Mzigo ulio mabegani ni mzito lakini mtu wa Mungu ninayejua, utawezana Jakwath. Mungu akupe nguvu, uvumilivu na faraja baba Nyithindo. Tunakupenda mpenzi," Alisema.

Mwanamuziki huyo alisisitiza kuwa familia ya kina Jared itasalia kuwa familia yake kwa kuwa aliwahi kuoelewa kule na kupata watoto. 

Alifichua kuwa familia yake, baba na mama yake pia walihudhuria mazishi hayo na kufariji wakwe hao wao.

"Mama yangu anampenda Jared na hakuna kitu ninachoweza kumwambia kuhusu mkaza mwanawe. Poleni," Akothee alisema.

 Aliwasihi watu kuendeleza upendo na umoja katika familia zao badala ya chuki na mtawanyiko.