Unaweza kumtambua? Mtangazaji Gidi afufua kumbukumbu maalum ya wakati akiwa mwimbaji matata

Kundi la Gidi Gidi Maji Maji liliibuka na nyimbo maarufu zikiwemo 'I am Unbwogable,' Ting’ Badi Malo na Nyako Aheri.

Muhtasari

•Gidi alishiriki picha yake, Maji Maji na mwanasiasa John Kiarie ambaye wakati huo alikuwa mchekeshaji akijitambulisha kama KJ.

•Kundi la muziki la Gidi Gidi Maji Maji lilitengana hapo mwaka wa 2005 ambapo Gidi baadaye alijiunga na shirika la UNEP.

katika picha ya maktaba.
Gidi Gidi, KJ, Maji Maji katika picha ya maktaba.
Image: FACEBOOK// JOE GIDI

Siku ya Ijumaa, mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi kwenye Radio Jambo, Joseph Ogidi Oyoo almaarufu Gidi alishiriki kumbukumbu ya miaka mingi iliyopita wakati alipokuwa mwanamuziki matata.

Miaka mingi kabla ya kuwa mtangazaji wa redio, Gidi alikuwa kwenye tasnia ya muziki ambapo yeye na mwanasiasa Julius Owino almaarufu Maji Maji walianzisha kundi la muziki la Gidi Gidi Maji Maji ambalo liliibuka na nyimbo maarufu zikiwemo I am Unbwogable, Ting’ Badi Malo na Nyako Aheri.

Ijumaa, Gidi alitumia kurasa zake za mitandao ya kijamii kufufua kumbukumbu za takriban miongo miwili iliyopita kwa kushiriki picha yake, Maji Maji na mwanasiasa John Kiarie ambaye wakati huo alikuwa mchekeshaji akijitambulisha kama KJ. Kwenye picha hiyo, alibainisha kuwa kweli wametoka mbali kufika mahali walipo sasa.

"Mhesh John Kj Kiarie, hii TBT ni ya power, imekuwa safari kweli," Gidi aliandika kwenye sehemu ya maelezo ya picha hiyo.

Picha ambayo mtangazaji huyo wa redio alichapisha, kuna uwezekano mkubwa ilipigwa kati ya mwaka wa 2002 na 2003 wakati wimbo wao 'I am Unbwogable' bila shaka ulikuwa wimbo mkubwa zaidi nchini. Mashati meupe waliyovaa Gidi na Maji Maji kwenye picha hiyo yalikuwa na maandishi ya jina la wimbo wao ‘I am unbwogable.’

Kundi la muziki la Gidi la watu wawili lilitoa wimbo wa 'I an Unbwogable' wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2002. Rais wa zamani, hayati Emilio Mwai Kibaki alikuwa ametumia wimbo huo sana katika kampeni zake na bila shaka ukawa wimbo wake wa utambulisho.

Mwaka jana, mtangazaji huyo mahiri alifichua kuwa licha ya wimbo wao kutumiwa sana na Narc wakati wa kampeni, hawakuwahi kupata fidia yoyote kutoka kwa chama hicho. Alisema hata hivyo walitumia fursa hiyo kutengeneza t-shati nyingi zenye maandishi ‘I am unbwogable’ ambazo waliuza wakati wa mikutano ya kisiasa.

"KANU ilitaka kuununua wimbo huo lakini tukakataa, haukuwa wetu tena bali ulikuwa wimbo wa Taifa wa mapambano ya watu wakati huo. Ulikuwa ni wakati UNBWOGABLE," Gidi alisema.

Kundi la muziki la Gidi Gidi Maji Maji lilitengana hapo mwaka wa 2005 ambapo Gidi baadaye alijiunga na shirika la UNEP na kufanya kazi hapo kwa muda kabla ya kuwa mtangazaji katika Radio Jambo.