Vybz Kartel aonyesha sura yake mpya baada ya jela, ajitahidi kurejesha afya ya mwili (+picha)

Ameeleza kwamba amekuwa akitumia siku chache zilizopita za uhuru wake na familia huku akijaribu kurejesha ufya yake.

Muhtasari

•Msanii huyo alichapisha video inayomuonyesha akiongea na mashabiki wake baada ya kipindi cha mazoezi ya asubuhi.

•Staa huyo wa  dancehall aliendelea kupigia debe afya na familia, akibainisha kwamba ndivyo  vitu kuu zaidi maishani.

Image: HISANI

Mwimbaji maarufu wa dancehall kutoka Jamaica Adidja Palmer almaarufu Vybz Kartel ameonyesha wazi video na picha za muonekano wake mpya siku chache baada ya kutoka gerezani.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 48 aliachiliwa kutoka jela wiki iliyopita baada ya kufungiwa kwa takribani miaka kumi na tatu na picha za kuhofisha zimekuwa zikivuma kwenye mitandao ya kijamii, huku watumiaji wa mtandao wakiibua maswali chungu nzima kuhusu sura yake tofauti kabisa.

Siku ya Jumanne, Kartel alichapisha video inayomuonyesha akiongea na mashabiki wake baada ya kipindi cha mazoezi ya asubuhi.

"Ndio watu, nimemaliza mazoezi yangu ya asubuhi. Tunafanya kitu kimoja kwa wakati mmoja, siwezi kuzidisha bado, tunachukua hatua kwa hatua," Vybz Kartel alisema kwenye video aliyoichapisha kwenye Instagram.

Staa huyo wa nyimbo za dancehall aliendelea kupigia debe afya na familia, akibainisha kwamba ndivyo  vitu kuu zaidi maishani.

"Afya na familia, Mungu ndiye mkuu," alisema.

Pia alichapisha  picha zingine zake akiwa amekaa kwenye sofa nyumbani kwake na akaeleza jinsi anavyojisikia vizuri kuwa huru.

"Mtaa wa Uhuru #GodistheGreatest," alisema.

Machapisha ya hivi majuzi ya staa huyo wa dancehall yanaonyesha kuwa amekuwa akitumia siku kadhaa zilizopita za uhuru wake akitangamana na familia yake na akijaribu kujiweka fiti tena.

Mnamo Julai 31, 2024, Kartel na washtakiwa wenzake watatu waliachiliwa kutoka gerezani kwa uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Rufaa ya Jamaica.

Mashabiki kutoka kote ulimwenguni walisherehekea kuona mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 48 akiungana na familia yake na marafiki baada ya kufungwa kwa takriban miaka 13. Amekuwa gerezani tangu 2011 baada ya kupatikana na hatia ya mauaji ya Clive "Lizard" Williams.

Wakati wa kuachiliwa kwake, alikutana na umati wa wafuasi ambao walimshangilia wakati akitoka gerezani. Hata hivyo, alikuwa amevaa miwani ya jua na kanga ili kuficha uso wake.

Hata hivyo baadaye, picha na video za wazi za msanii huyo ziliibuka zikionyesha jinsi uso na shingo yake ilivyovimba, jambo ambalo lilizua wasiwasi miongoni mwa mashabiki wake.

Inaripotiwa kuwa nyota huyo wa dancehall amekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa Graves na ugonjwa mbaya wa moyo, ambao ulizingatiwa wakati wa kuachiliwa kwake.

 Wakati wa uamuzi huo, iliamuliwa kwamba ugonjwa wa Graves ulitoa hatari ya wazi na ya sasa kwa ustawi wa Vybz, ambayo inaonekana iliimarisha uamuzi wa kuachiliwa kwake.

Ugonjwa wa Graves, ni hali ya mfumo wa kinga ambayo husababisha mwili kutoa homoni nyingi za tezi, kulingana na Kliniki ya Mayo. Ugonjwa huo unaweza kusababisha ugonjwa wa jicho la tezi, unaonyeshwa na macho makali.

Zaidi ya hayo, Vybz pia anaugua ugonjwa wa moyo.