Zuchu atamani kuwa mrembo wa taifa baada ya kuchochewa na akina Wema Sepetu

Mwimbaji huyo ameweka wazi ndoto yake kuwa Miss Tanzania siku moja.

Muhtasari

•Zuchu alibainisha kuwa kutwaa taji la Miss Tanzania ni ndoto ya wanadada wengi kwenye fani ya urembo ya nchi hiyo.

•Binti huyo wa Khadija Kopa alitumia fursa hiyo kuwapongeza mrembo wa taifa wa sasa, Halima Kopwe na wale wa zamani.

Image: INSTAGRAM// ZUCHU

Malkia wa muziki wa Bongo Zuhura Othman almaarufu Zuchu ameweka wazi ndoto yake kuwa Miss Tanzania siku moja.

Katika taarifa yake ya  siku ya Jumatatu, msanii huyo wa WCB alibainisha kuwa kutwaa taji la Miss Tanzania ni ndoto ya wanadada wengi kwenye fani ya urembo ya nchi hiyo.

"Naamini kila mrembo hutamani siku moja kuja kuwa mrembo wa Taifa. Ukiamini katika ndoto zako na ukazipambania, kamwe hautoweza kufeli kila jambo linawezekana kwa kupambana na kumuomba Mungu," alisema.

Binti huyo wa gwiji wa taarab Khadija Kopa alitumia fursa hiyo kuwapongeza mrembo wa taifa wa sasa, Halima Kopwe na wale wa zamani wakiwamo muigizaji Wema Sepetu, Jacqueline Mengi, Nancy Sumari, Elizabeth Makune na wengineo.

Aliambatanisha ujumbe huo na picha zake akiwa amevalia gauni nyeupe na mshipi wa Miss Tanzania. Kichwani pia alivalia taji.

Haya yanajiri katika kipindi ambacho mwimbaji huyo wa kibao ‘Sukari’ amejikita kwenye muziki wake baada ya kutengana na bosi wake Diamond. Mwezi uliopita, wawili hao walitangaza kuwa mahusiano yao yamefika mwisho.

Katikati mwa mwezi Febuari, Zuchu aliibua wasiwasi kuhusu hali ya mahusiano yake kufuatia chapisho lake kwenye Snapchat.

Mwanamuziki huyo wa lebo ya WCB alidokeza kwamba amevunjwa moyo na mpenzi wake na kutangaza kuwa yuko single.

"Single.." aliandika na kuambatanisha na emoji ya moyo uliovunjika '💔'

Binti huyo wa Khadija Kopa pia alichukua hatua ya kufuta picha zote za bosi wake Diamond kwenye mtandao wa Instagram.

Baadaye, Diamond alizamia kwenye mtandao wa Instagram kuthibitisha kutengana na binti huyo wa Khadija Kopa.

Katika taarifa yake, bosi huyo wa WCB aliweka wazi kwamba yeye na Zuchu sio wapenzi tena. Alibainisha kuwa yeye na malkia huyo wamebaki kuwa kaka na dada licha ya awali kuonyesha mahaba makubwa  kati yao.

"Kwa pamoja na Zuhura tunaomba tuwataarifu ya kwamba, kwa sasa sisi ni dada na kaka na si wapenzi kama ilivyokuwa ikidhaniwa ama wengine kujua.. Mnaruhusiwa wachumba na wake ama waume kama tutawaridhia," alisema.

Diamond aliongeza, "Lakini muwe na vibarua vinavyoeleweka  sio mje kutuchuna, maana atuhongi hovyo."