Mr Seed avunja kimya baada ya mkewe kumkashifu hadharani kufuatia matamshi ya kutatanisha

Mwanamuziki huyo amebainisha kwamba alieieweka vibaya na alihukumiwa vibaya kuhusu kauli zake za hivi majuzi.

Muhtasari

•Huku akijitetea kupitia Instagram siku ya Jumanne mchana, mwanamuziki huyo alikosoa jinsi watu walivyomwelewa na kumhukumu.

•Mr Seed alisema wanaume kwa kawaida ni wa mitala na kwamba mwanamke kuishi na yeye kwa muda mrefu si kigezo cha kumfanya kuhisi kwamba ameshinda.

Nimo Gachuiri na mumewe Mr Seed
Image: INSTAGRAM// MR SEED

Mwimbaji maarufu wa nyimbo za Injili wa Kenya Moses Omondi almaarufu Mr Seed amebainisha kwamba hakueleweka na alihukumiwa vibaya kuhusu kauli zake za hivi majuzi.

Msanii huyo wa zamani wa EMB Records katika kikao cha podikasti cha hivi majuzi alirekodiwa akitoa maoni ya kutatanisha kuhusu wanaume kuwa na wapenzi wengi, maoni ambayo yamemweka matatani hata na mke wake Nimo Gachuiri ambaye tayari amemkashifu hadharani na kuacha kumfuatilia kwenye mtandao wa Instagram.

Huku akijitetea kupitia Instagram siku ya Jumanne mchana, mwanamuziki huyo alikosoa jinsi watu walivyomwelewa na kumhukumu.

"Nimeeleweka vibaya na nimehukumiwa. Anyway nabariki spika zenu hivi karibuni. Endelea kuwa nasi!!” Mr Seed alisema.

Msanii huyo mahiri alitokea kwenye podcast moja ya humu nchini na kuzungumzia masuala ya mahusiano ambapo aliweka wazi kwamba  kwa tajriba yake kwenye ndoa, mwanamume ni kiumbe ambaye anaweza akawa kwenye mahusiano na mwanamke kwa miaka 3 lakini bado akawa anawazia kuoa mwanamke mwingine.

Mr Seed alisema kwamba wanaume kwa kawaida ni wa mitala na kwamba mwanamke kuishi na yeye kwa muda mrefu si kigezo cha kumfanya kuhisi kwamba ameshinda, kwani anaweza amka siku moja tu agundue mume wake anapanga kufunga harusi na mwanamke mwingine hali ya kuwa yeye bado yupo.

“Hebu niambie, sisi wanaume tuna akili. Ninaweza kuwa na wewe kwenye uhusiano kwa miaka kama 3 unaelewa? Miaka mitatu tu ya mimi kukutazama nikijua vizuri huna ninachokitaka.”

“Kwa hivyo niko hapo halafu siku moja unaamka na kukuta jamaa tayari ameshaandaa harusi kwa sababu msichana huyu tayari alidhani alikuwa mshindi. Tuna marafiki wengine wa kike sawa? Miongoni mwa marafiki hao, tunaangalia kati yao kuona nani ni mke mzuri. Labda hata ni rafiki yako mkubwa,” Mr Seed alisema.

Aliongeza "Wanaume wameumbwa kuwa na wake wengi."

Matamshi haya yalionekana kumuudhi mno mkewe Nimo ambaye kupitia Instastori zake alimkanda vikali akisema kwamba matamshi kama hayo hayafai kutoka kwa kinywa cha mwanaume anayejua kwamba yuko katika ndoa imara.

"Kwa hivyo niliona kipande kidogo cha podikasti iliyofanywa na Mr Seed, akisema chochote alichokuwa akisema. Hata sikumaliza kuitazama. Nilikasirika. Basi nikamgeukia na kumuuliza, hizi sasa ni nini unasema hakika. Kitu kingine nilichosema lazima watu wafikiri mimi ni mjinga! Kwa hivyo alikuwa kama unapaswa kutazama podikasti nzima na walichagua sehemu hiyo pekee ili iweze ku-trend,” Nimo aliandika.

"Ninachotaka kusema ni kama ni kwa ajili ya mapenzi, lilikuwa jambo lisilo na hisia kusema wakati uko katika uhusiano wa kujitolea," alisema zaidi.

Kwa tathmini ya haraka, Nimo alikuwa tayari ameshakatisha urafiki kwa mumewe katika mtandao wa Instagram.