"Msichoke na Mimi" Akuku Danger awasihi Wakenya kumsaidia kulipa bili zake za hospitali

Muhtasari

•Akuku amekuwa akipokea matibabu katika hospitali ya Nairobi West baada ya kulazwa takriban wiki mbili zilizopita. 

• Akuku amesema kulazwa hospitalini mara nyingi mwaka huu kumemdhoofisha kiakili, kifedha na kimwili.

Akuku Danger
Image: Radiojambo

Mchekeshaji Mannerson Oduor almaarufu Akuku Danger ametoa wito kwa Wakenya kumsaidia kulipa  bili zake za hospitali.

Akuku amekuwa akipokea matibabu katika hospitali ya Nairobi West baada ya kulazwa takriban wiki mbili zilizopita. 

Jumanne, mwandani wake Sandra Dacha alifichua kwamba amepata nafuu na tayari ameruhusiwa kwenda nyumbani ila hospitali ilikuwa imemzuia kutokana na salio la bili ya Sh883,000.

"Hospitali imekataa kupokea dhamana ili Akuku apange malipo akiwa nje licha ya kuwa na dhamana yao kutoka Januari ambayo ni ya thamani ya juu kuliko bili yote. Yeyote aliye tayari kusaidia kwa njia yoyote tafadhali atufikie," Dacha alisema kupitia Instagram.

Jumatano, Akuku alisema kulazwa hospitalini mara nyingi mwaka huu kumemdhoofisha kiakili, kifedha na kimwili.

Ameeleza kwamba ugonjwa wa Sickle Cell Anemia ambao alizaliwa nao ndio umekuwa ukimwathiri kiasi cha kulazwa.

"Imekuwa changamoto lakini bado ninashikilia. Msichoke na Mimi," Akuku amewaomba Wakenya.

Amewataka Wasamaria wema ambao wangependa kumsaidia kutuma mchango wao kwa Paybill Namba 8024409, Akaunti: AKUKU MEDICAL FUND.

Jumanne Hospitali ya Nairobi West ilithibitisha kwamba  Akuku anazuiliwa katika kituo chao kufuatia salio la bili.

 Akizungumza katika mahojiano ya simu Jumanne, Mkuu wa Mawasiliano ya Umma Habil Okumu alisema hospitali haiwezi kufichua habari zaidi kuhusu mgonjwa yeyote kwa sababu za kisheria.

Katika kutetea hatua yao ya kumzuilia mcheshi huyo, Okumu alisema hospitali hiyo pia ina bili za kulipa

 “Tuna wauguzi na wafanyakazi wanaohitaji kulipwa. Kwa upande wa huduma, Akuku hatari alisaidiwa alipokuja. Lakini tunataka kutekeleza usiri wa mgonjwa na hospitali hadi tutakapotoa taarifa rasmi kuhusu kuzuiliwa kwake,” alisema. 

Mwaka huu mchekeshaji huyo amelazwa hospitalini na kutoka mara  kadhaa, jambo ambalo limemwathiri kifedha.