Mchekeshaji maarufu wa Kenya David Oyando almaarufu Mulamwah hatimaye amejibu kuhusu tetesi za awali za harusi iliyodaiwa ya aliyekuwa mpenzi wake, Caroline Muthoni.
Mapema mwezi huu, muigizaji Carol Muthoni ambaye anajulikana zaidi kama Carrol Sonnie alikuwa amedokeza kwamba angefunga ndoa mnamo Januari 6, 2024.
Mama huyo wa binti mmoja alitumia ukurasa wake wa Instagram kudokeza kuhusu hatua hiyo kubwa na kumshukuru Mungu kwa fanikio hilo muhimu.
"Januari 6 ndio. Mungu amekuwa mwaminifu. Je, umealikwa?,” Sonnie aliandika kwenye Instastories zake.
Pia aliambatanisha ujumbe huo kwa emojis za moyo na za pete ambazo mara nyingi hutumiwa kuashiria mapenzi au harusi.
Wakati Mulamwah alikuwa akiwashirikisha mashabiki wake katika kipindi cha maswali na majibu siku ya Alhamisi asubuhi, mtumiaji mmoja wa Instagram alitaka kujua kwa nini baba huyo wa binti mmoja hakuhudhuria harusi hiyo iliyodaiwa.
“Niliskia 6th kulikuwa na harusi, hukuenda?” shabiki mmoja alimuuliza Mulamah.
Katika jibu lake, mchekeshaji huyo ambaye anatarajia mtoto wake wa pili alibainishakuwa hakuwa na habari kuhusu madai ya harusi hiyo.
Hata hivyo aliomba kufahamishwa ikiwa harusi hiyo ilikuwepo na akaendelea kuifanyia mzaha.
"Sikujua, lakini ikiwa mnishow nijifunge mkanda wa usalama incase DUNIA isimame ghafla," mchekeshaji huyo alijibu.
Mulamwah na mzazi mwenzake Carrol Sonnie walitengana mwezi Desemba 2021, takriban miezi mitatu baada ya kuzaliwa kwa binti yao Keilah Oyando.
Tangu kutengana kwao, wawili hao hawajakuwa na uhusiano mzuri na hata wamewahi kutupiana cheche za maneno hadharani mara kadhaa.