Mwanamuziki Nadia Mukami ahusika katika ajali ya barabarani

Mwimbaji huyo alisema ana bahati ya kunusurika kwenye ajali hiyo aliyotaja kuwa shambulio la kiroho.

Muhtasari

•Nadia Mukami alinusurika kifo siku ya Jumapili baada ya kuhusika katika ajali ya barabarani katika eneo lisilobainishwa.

Leo ilikuwa ya kutisha. Ajali zinatisha sana. Lakini namshukuru Mungu kwamba niko hai na niliweza kwenda nyumbani kwa mwanangu,” alisema.

Image: INSTAGRAM// NADIA MUKAMI

Malkia wa muziki wa Kenya Nadia Mukami alinusurika kifo siku ya Jumapili baada ya kuhusika katika ajali ya barabarani katika eneo lisilobainishwa.

Katika taarifa ya video aliyotoa Jumapili jioni, mchumba huyo wa mwimbaji Arrow Bwoy alisema ana bahati ya kunusurika kwenye ajali hiyo aliyotaja kuwa shambulio la kiroho.

“Sijawahi kupitia tukio kama hilo. Ninamshukuru Mungu tu kwamba niko hai. Leo nahisi ni kama shambulio la kiroho, naapa kwa Mungu,” Nadia alisema.

Mwimbaji huyo aliendelea kusimulia jinsi ajali hiyo ilivyotokea akifichua kuwa kulikuwa na athari kubwa kwa gari lake kufuatia ajali hiyo.

“Tulipata ajali. Tulikuwa sehemu tofauti tukielekea upande mmoja na ajali ilitokea kwa wakati mmoja, ni mbaya kiasi gani. Sisi tuliponea. Ikiwa ingekuwa trela labda nisingekuwa hai. Nashukuru ilikuwa gari ndogo kwa sababu athari kwenye gari ni kubwa sana,” alisema.

Nadia alifichua kuwa licha ya yeye na wengine waliokuwa ndani ya gari ambalo alikuwemo kunusurika, dereva aliyekuwa kwenye gari hilo lingine aliachwa na majeraha mabaya sana.

"Yuko katika hali mbaya sana, hali mbaya sana. Siwezi hata kueleza hilo. Leo ilikuwa ya kutisha. Ajali zinatisha sana. Lakini namshukuru Mungu kwamba niko hai na niliweza kwenda nyumbani kwa mwanangu,” alisema.

Mama huyo wa mvulana mmoja alifichua kwamba alifika nyumbani usiku wa Jumapili kwani kwanza alipitia hospitali baada ya ajali hiyo.

"Nimekuwa hospitalini na yule jamaa mwingine. Jamaa huyo mwingine bado yuko hospitalini," alisema.

Mwimbaji huyo alirekodi taarifa hiyo ya video huku akiwa amelala kitandani mwake na kuisambaza kupitia ukurasa wake wa Instagram.