"Najiskia vibaya!" Wema Sepetu alalamikia kudhihakiwa kwa kushindwa kupata watoto

Wema alikiri kuwa kudhalilishwa kwa kutofanikiwa kuzaa imekuwa ikimuumiza kila mara.

Muhtasari

•Wema amewakosoa watu ambao wamekuwa wakimdhihaki lakini akawabainishia kuwa kejeli zao hazijamfanya apoteze matumaini.

•Wema alichapisha picha yake akiwa ameshika mtoto mchanga na kusema jambo hilo lilimfanya atamani kuwa na mtoto wake.

Image: INSTAGRAM// WEMA SEPETU

Muigizaji maarufu wa Bongo Wema Sepetu amevunja kimya kuhusu dhihaka nyingi ambazo amekuwa akikumbana nazo kwa kutokuwa na watoto wake.

Akizungumza kupitia ukurasa wake wa Instagram, Wema Sepetu alikiri kuwa kudhalilishwa kwa kutofanikiwa kuzaa imekuwa ikimuumiza kila mara.

Kwa hilo, amewakosoa watu ambao wamekuwa wakimdhihaki lakini akawabainishia kuwa kejeli zao hazijamfanya apoteze matumaini.

"Alafu sikieni niwaambie, msione kwamba basi mkiniambia nimekosa mtoto basi ndo mnaniweeeeeza!!" alisema.

"Sawa naumia sikatai na mjue nitazoea. Sema mnaboa!!! Mnaudhi...!!! Najiskia vibaya!!! Sipendi!!!" 

Haya yanajiri siku chache tu baada ya mpenzi huyo wa zamani wa Diamond kumuomba Maulana amjalie mtoto wa kwake siku moja.

Wiki jana, Wema alichapisha picha yake akiwa ameshika mtoto mchanga na kusema jambo hilo lilimfanya atamani kuwa na mtoto wake.

"Eh Mungu tafadhali nibariki na wangu siku moja🙏🙏🙏," alisema.

Wema alikiri kuwa kumtazama mtoto huyo mchanga mikononi mwake kulimfanya ajisikie kuwa kuenda naye awe wake.

"Nilitamani nikimbie naye wallahy🥺🥺🥺" alisema.

Kwa miaka mingi, muigazaji huyo amekuwa akishambuliwa na kukejeliwa mitandaoni kutokana na hali yake. Wengine hata hivyo wamekuwa wakimfariji na kumtia moyo mpenzi huyo wa zamani wa Diamond.

Takriban miaka minne iliyopita Wema aliwahi kufunguka kuhusu  tatizo kwenye tumbo lake la uzazi linalomzuia kushika ujauzito.

“Unajua mimi nilikuwa na tatizo kubwa sana kwa upande wa tumbo langu la uzazi lililosababisha nisiweze kuzaa kwa muda wote huu. Ngoja niweke wazi leo watu wajue, mimi nina ugonjwa ambao unasababisha mayai yangu ya uzazi kutoboka na kushindwa kupevusha mbegu za uzazi," Alisema katika mahojiano na Global Publishers.

Licha ya kuwa na tatizo kwenye tumbo la uzazi, muigizaji huyo mwenye sauti nzuri kweli amekuwa akionyesha wazi kuwa bado hajapoteza matumaini ya kuwahi kukumbatia mtoto wake kuzaa katika siku za usoni.

Siku chache zilizopita, anayeaminika kuwa mpenzi wake wa sasa Whozu alishiriki mahojiano na wanahabari ambapo alithibitisha kuwa ni kweli alikuwa amempachika mimba muigizaji huyo ila kwa bahati mbaya ikaharibika.

Mwanamuziki huyo alieleza kusikitishwa kwake na watu waliotilia shaka habari za yeye kumpachika mimba mpenziwe.

"Iliniuma. Alafu watu wanafikiria ni uwongo! Mnanionaje kuwa mimi siwezi kumpa mtu mimba? Mnanichukuliaje?,"  alisema.

Alidokeza kuwa anapanga kumpachika Wema ujauzito kwa mara nyingine baada ya ule wa kwanza kutofikia hatua ya kujifungua.

Whozu alisema kuwa  yeye na mpenziwe wanatamani kupata mtoto wa kiume pamoja.

"Lazima niweke pale. Lazima kuwa na Lola na mdogo wake Lola. Naomba Mungu awe wa kiume. Mamake atakuwa Wema Sepetu," alisema.

Mwimbaji huyo alisema kuwa bado anafanya juhudi nyingi na pia anamuombea sana mpenzi wake apate ujauzito tena.