"Najivunia kuitwa mamako" Diana Marua amthibitishia upendo Morgan Bahati kufuatia uhasi mitandaoni

Diana alithibitisha kuwa anajivunia kuwa na mvulana huyo wa miaka 13 kama mwanawe.

Muhtasari

•Diana alisema kwamba yeye na mume wake kuwa na Morgan katika familia yao kulikuwa na matokeo chanya katika maisha yao.

•Pia alimshukuru mume wake Bahati kwa kusimama na familia yake na akamhakikishia upendo wao mkubwa kwake.

amemhakikishia upendo Morgan Bahati kufuatia mashambulizi mitandaoni.
Diana Marua amemhakikishia upendo Morgan Bahati kufuatia mashambulizi mitandaoni.
Image: INSTAGRAM// DIANA MARUA

Mwanavlogu Diana Marua amekiri upendo upendo wake mkubwa kwa mwanawe wa kulea Morgan Bahati siku chache tu baada ya mashambulizi ya mitandao ya kijamii.

Wakati akijibu barua ndefu ya mume wake Bahati kwa Morgan kwenye Instagram, Diana alithibitisha kuwa anajivunia kuwa na mvulana huyo wa miaka 13 kama mwanawe.

Mama huyo wa watoto watatu alisema kwamba yeye na mume wake kuwa na Morgan katika familia yao kulikuwa na matokeo chanya katika maisha yao.

“Nimebarikiwa kuitwa Mama yako. Wewe ndiye uliyenitungulia milango mingi mimi na Baba yako. Siku ambayo Baba yako alikuchukua, Mbingu ilitabasamu juu ya maisha yake na Baraka zitamfuata milele. Ninajivunia kuitwa Mama yako," Diana aliandika.

Aidha, mke huyo wa mwimbaji Bahati alichukua nafasi hiyo kumuahidi Morgan kuwa ataendelea kumpenda na kumtaka ajivunie maishani.

Pia alimshukuru mume wake Bahati kwa kusimama na familia yake na akamhakikishia upendo wao mkubwa kwake.

“Mungu alikuchagua kwa ajili yetu nasi tutakupenda MILELE! Mungu aendelee kukuzidishia, asante kwa yote uliyotutendea. TUNAKUPENDA @bahatikenya,” alisema.

Jumatano jioni, Bahati aliandika barua ndefu kwa  Morgan Bahati ambapo alimhakikishia kijana huyo mwenye umri wa miaka 13 kwamba yeye ndiye babake licha ya maneno yote hasi ambayo yamesemwa kwenye mitandao ya kijamii.

Kuthibitisha kujitolea kwake na upendo wake kwa mvulana huyo,Bahati alichukua fursa hiyo kusimulia safari ndefu ambayo wametembea pamoja tangu amchukue kutoka kwa nyumba ya watoto takriban miaka kumi iliyopita.

"Nimeitazama picha hii na nikagundua kuwa unakuwa Mwanaume. Hii ni miaka 10 iliyopita, siku ya kwanza nilipokutana nawe. Siku hiyo nilipoalika ABC Children's Home (ambapo nilikulia) kuja na kutumbuiza katika Uzinduzi wa Albamu yangu mwaka wa 2013 katika NPC Valley Road. Mwana nakumbuka siku ile kama Jana; jinsi ulivyolia na kuniita baba. Ilikuwa ngumu sana kwangu kuona wewe ukiwa na miaka 2 ukilazimisha kuingia kwenye basi linalorudi kwenye kituo cha watoto yatima; Niliona uchungu wako na nikajiona kupitia kwako; Kwa kuwa nimekua katika Nyumba ya Watoto wakati fulani, nikiwa pweke bila mtu wa Kumwita Mama au Baba!,” Bahati alisimulia chini ya picha zilizoonyesha ukuaji wa Morgan tangu walipokutana kwa mara ya kwanza hadi sasa.

Akaendelea, ” Mwanangu tangu siku ile; ingawa sikuwa tayari niliamua kuwa baba na nikakuchukua kama mwanangu. Mwana Nisikilize! Mimi ni Baba yako na Wewe ni Mwanangu! Mungu Alipanga Hakuna Kitu Kinachoweza Kubadili Hilo! Unapokua utaona mambo mengi ya Upuuzi na ya kinyama yanayosemwa kwenye Ulimwengu huu usio na huruma lakini kila wakati kumbuka licha ya yote, MIMI NI BABA YAKO NA WEWE NI MWANANGU! Mungu pekee ndiye Ajuaye yale tuliyopitia.”

Bahati alitumia fursa hiyo kufunguka kuhusu baadhi ya misukosuko aliyopitia kijana huyo mdogo ikiwa ni pamoja na kutomudu kodi ya nyumba na kulazimika kusafisha nguo zake wakati hakuwa na uwezo wa kulipa msaidizi wa nyumbani.

Pia alifichua kuwa baadhi ya wanawake aliotaka kujenga nao familia walimuacha kwa kuwa hawakuwa tayari kulea watoto ambao hawakuzaa. Hata hivyo alielezea furaha yake kwa kukutana na Diana Marua ambaye alimkumbatia kama mwanawe na kumuonyesha upendo.

Kufuatia mashambulizi ya hivi majuzi kwenye mitandao ya kijamii, mwimbaji huyo wa nyimbo za mapenzi alichukua lawama zote na kumuomba msamaha kijana huyo wa miaka 13 kwa kumtambulisha hadharani.

"Nisamehe kwa kukutambulisha kwa umma kijana wangu. Lakini juu ya yote nataka Ujue kuwa Wewe ndiye Zawadi Bora kabisa ambayo nimewahi kupata – Wewe ndiye  mzaliwa wangu wa kwanza na bila wewe familia yetu haijakamilika," aliandika.

Bahati pia alimhakikishia mwanawe kuhusu upendo wake mkubwa kwake na kuahidi kumuunga mkono ili kufikia ndoto zake zote.