"Nawamiss sana!" Akothee awaza kustaafu ili kuwa na wanawe wanaoishi Ufaransa

"Ninawamiss sana watoto wangu, huenda nikalazimika kustaafu ili kuacha kufanya kazi na kuwa nao tu," alisema.

Muhtasari

•Akothee amekuwa akifurahia muda na wanawe wawili, Prince Ojwang na Prince Oyoo katika siku chache zilizopita.

•Akothee alionekana kuguswa sana na kipindi hicho na akafichua jinsi anavyotamani kuwa na wakati zaidi na wanawe.

Akothee na wanawe Prince Oyoo na Prince Ojwang
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwanamuziki wa Kenya Akothee amekuwa akifurahia muda na wanawe wawili, Prince Ojwang na Prince Oyoo katika siku chache zilizopita.

Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 43 aliwatembelea wawili hao ambao wanaishi na baba mtoto wake wa mwisho nchini Ufaransa wiki iliyopita kabla ya kuelekea Switzerland ambako atakutana na mume wake Denis Shweizer.

Siku ya Jumanne, alionyesha video yake na mwanawe Prince Ojwang katika mkahawa ambapo walipata vinywaji.

"Nimeenda kupata kinywaji na mwanangu," Akothee alisema kwenye video hiyo.

Huku mwanawe akiagiza maji ya moto na sukari, mama huyo wa watoto watano alitoa mfuko mdogo wa chai ya Kenya aliyokuwa amebeba mfukoni na kuongeza kwenye maji moto ambayo alikuwa ameagiza.

"Chai ya Kenya rafiki yangu. Itapata njia tu," alisema.

Katika video nyingine, mwimbaji huyo alionekana akishiriki mazungumzo na mwanawe ambapo alimweleza kuhusu ratiba ya ziara yake.

Alifichua kwa mwanawe kuhusu mipango yake ya kwenda kufurahia fungate na mumewe kabla ya kuwa nao tena.

“Sasa nitaenda honeymoon kisha nitarudi. Nitakuwa hapa tarehe 9 kisha nitakaa na nyinyi kwa angalau siku tano kisha nitalazimika kurudi Kenya kwa ajili ya kazi," alisema.

Ojwang ambaye alionekana kutamani kuwa na muda zaidi na mama yake hakuwa na budi ila kumuelewa na kukubaliana naye.

Akothee alionekana kuguswa sana na kipindi hicho na akafichua jinsi anavyotamani kuwa na wakati zaidi na wanawe. Kufuatia hilo, alidokeza kwamba huenda akawaza kustaafu kazi yake ili tu kuwa nao.

"Ninawamiss sana watoto wangu, huenda nikalazimika kustaafu ili kuacha kufanya kazi na kuwa nao tu," alisema.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Takriban wiki mbili zilizopita, mwanamuziki huyo alifichua kuwa mume wake Denis Shweizer almaarufu Omosh alimwagiza aache kazi, aondoke kwenye mitandao ya kijamii na aondoke Kenya ili kuwa naye.

Pia alitangaza mpango wake wa kuchukua mapumziko kutoka kwa mitandao ya kijamii huku akieleza kwamba madhumuni ya mapumziko hayo ya muda usiobainishwa yatakuwa kuangazia kuongeza mtoto mwingine.

Aliwaomba mashabiki wake wamruhusu achukue mapumziko akisema anataka kupata mtoto wake wa sita hivi karibuni.

"Sasa nyie mnipe muda. Nitapumzika kutoka kwa kila mtu na kila kitu pamoja na mitandao ya kijamii. Mniruhusu nitafute mtoto wangu wa pili kutoka mwisho, kabla hatujazungumza mambo mengine.  Nataka kuwa mama mwaka huu," Akothee alisema kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram.