Staa wa Bongofleva, Naseeb Abdul Juma almaarufu Diamond Platnumz ametangaza rasmi kuwa yuko single.
Katika taarifa yake usiku wa kuamkia leo Alhamisi, mwimbaji huyo ambaye kwa muda mrefu imekuwa ikisemekana kuwa anatoka kimapenzi na msanii wake Zuhura Othman almaarufu Zuchu aliweka wazi kuwa hana uhusiano wa kimapenzi na mwanamke yeyote.
“Kuanzia leo ningependa niwatangaze rasmi kuwa I AM SINGLE, sidate wala sina mahusiano na mwanamke yeyote,” Diamond alisema kupitia Instagram.
Aliendelea kuwasihi mashabiki kuacha kumuwekea mpenzi yeyote akisema kuwa atakuwa wa kwanza kutangaza atakapoingia kwenye uhusiano.
“Hivyo nisiwekewe mwanamke yeyote kama mwanamke wangu, itakapotokea kudate ama kuwa na mahusiano nitawajuza ama kutambulisha kama jinsi huwa nafanya,” alisema.
Alitoa tangazo hilo kupitia instastori zake lakini akafuta baadaye.
Kauli hii inakuja siku chache tu baada ya mama mzazi wa bosi huyo wa WCB, Bi Sanura Kassim maarufu Mama Dangote kumkana hadharani Zuchu kuwa ni mkaza mwanawe. Kwa muda mrefu, Diamond na Zuchu wamekuwa wakidaiwa kuwa wapenzi na mara nyingi wamekuwa wakionekana wakishiriki nyakati za kimapenzi.
Katika mahojiano ya hivi majuzi na Wasafi Media, Mama Dangote alibainisha kuwa bosi huyo wa WCB hajawahi kumtambulisha Zuchu kama mpenzi wake.
Alibainisha kuwa anavyofahamu, binti huyo wa malkia wa taarab Khadija Kopa ni msanii tu chini ya lebo ya muziki ya Diamond Platnumz, Wasafi.
"(Diamond) hajawahi kuniletea Zuchu eti anataka kumuoa. Mimi kwanza najua Zuchu ni msanii wake," Mama Dangote alisema.
Aliongeza, "Kusema eti Zuchu ni mchumba wake sijui, kwa sababu mimi sijapeleka mahari kwa kina Zuchu wala barua. Zuchu namjua ni msanii wake. Kila siku tuko naye sijui. , najua ni msanii. Mimi ninachojua mchumba ni yule ambaye unapeleka barua na mahari."
Mama Dangote alidai kwamba mahusiano yanayodaiwa ya Diamond na msanii huyo wa kike wa WCB ni ya kuchezeana kwani hakuna taratibu za ndoa zilizofanyika.
“Kama mtu hajatoa barua, ni kutembea tu. Hiyo inaitwa kuchezeana. Huyo (Zuchu) sio mchumba, huyo ni mwanamke tu,” Mama Dangote alisema.
Pia alibainisha kuwa Zuchu si mwanamke wa kwanza kuhusishwa kimapenzi na mwanawe kwani amekuwa akidaiwa kutoka na wanawake wengine wengi waliowahi kuonekana naye katika siku za nyuma.
"Mimi najua mchumba Yule aliyeleta mahari," alisema.
Hata hivyo alisusia kujibu iwapo anaunga mkono uhusiano wa mastaa hao wawili wa bongofleva akibainisha kuwa wao wenyewe ndio wataamua.