"Nilijaribu kumuacha ila roho ikakataa!" Karen Nyamu afunguka kwa nini amemkwamilia Samidoh

Seneta Nyamu alisema alijaribu sana kumtema mwimbaji huyo lakini kila mara moyo wake bado ungemrudisha kwake.

Muhtasari

•Karen alisema alijaribu kusitisha mahusiano yao kutokana na shinikizo na huruma kwa mke wa kwanza wa Samidoh, Edday Nderitu.

•Akizungumzia sifa anazopenda kwa mpenziwe, Seneta Nyamu alimsifu na kufichua kuwa ana vibe ya kuvutia sana ambayo anaipenda.

Samidoh na Karen Nyamu
Image: HISANI

Seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu amefichua kwamba katika siku za nyuma alijaribu sana kumuacha mpenzi wake Samuel Muchoki almaarufu Samidoh bila mafanikio.

Akizungumza katika YouTube Channel ya Convo, Karen alisema kuwa hata kabla mambo yao hayajajulikana hadharani, alijaribu kusitisha mahusiano hayo kutokana na shinikizo na huruma kwa mke wa kwanza wa staa huyo wa Mugithi, Edday Nderitu.

Mama huyo wa watoto watatu alikiri kwamba aliamua kuacha mambo yakae kama yalivyo baada ya kujaribu kadri ya uwezo wake kusitisha uhusiano huo bila mafanikio.

“Ndivyo ilivyo (mahusiano), sasa kwa nini nipigane nayo, si kwamba sijawahi kujaribu kupigana nayo kwa sababu ya presha na nini na nini, na pia nikiwa mtu mzuri, kuna wakati ningeona hali hii ilivyo  si nzuri. Naona vipi kuhusu mtu mwingine? Naona si sawa," Karen Nyamu alisema.

Mwanasiasa huyo aliyezingirwa na drama si haba maishani alikiri kuwa kila alipotaka kuondoka, mapenzi mazito kwa Samidoh aliyoyabeba moyoni mwake yalikuwa yakimvuta arudi.

“Mambo ya roho! nilijaribu kuyapanga, nikasema mazee acha basi sasa iendelee kwa sababu nilijaribu nikashindwa,,” alisema.

Seneta huyo alifichua kuwa hata baada ya mahusiano yake na baba huyo wa watoto wake wawili kujulikana hadharani miaka michache iliyopita, alijaribu sana kumtema lakini kila mara moyo wake bado ungemrudisha kwake.

"Ogopa roho! Humjui vizuri!" alisema.

Alisema kuwa uhusiano wao ni muunganisho wa asili tu na akaweka wazi kwamba anafurahi juu yake. Pia alibainisha kuwa hayuko kwenye uhusiano kwa sababu ya pesa kwani wote si masikini.

Akizungumzia sifa anazopenda kwa mpenzi huyo wake, Seneta Nyamu alimsifu na kufichua kuwa ana vibe ya kuvutia sana ambayo anaipenda.

“Yupo poa, ana roho poa, anachekesha sana, ni muwazi, hajidai, roho iko uchi unaona. Ana vibe ambayo sijawahi kuona maishani mwangu. Anavutia sana. Kwa kawaida huwa anasema baadhi ya mambo na najua maishani mwangu sitawahi kusikia mtu mwingine akiyasema. Kwa kawaida mimi humwambia hivyo," Nyamu alisema.

Karen alifichua kwamba alikutana na Samidoh kwa mara ya kwanza katika hafla ambapo alikuwa akitumbuiza kabla ya kufahamiana vyema baadaye.

Samidoh na Karen Nyamu
Image: HISANI