"Nimefurahi wewe kuniita Mama" Diana Marua ajivunia mwanawe wa kulea, Morgan Bahati

Morgan alitimiza miaka 13 mnamo Desemba 22 mwaka jana.

Muhtasari

•Diana ameendelea kumsherehekea mwanawe Morgan Bahati, takriban wiki tatu baada ya siku yake ya kuzaliwa.

•Diana alisema ameona maendeleo na mabadiliko mengi kwa mwanawe na kumtakia mwongozo wa Mungu maishani.

Diana Marua na mtoto wake wa kulea Morgan Bahati.
Image: INSTAGRAM// DIANA MARUA

Mwanablogu wa YouTube Diana Marua ameendelea kumsherehekea mwanawe Morgan Bahati, takriban wiki tatu baada ya siku yake ya kuzaliwa.

Jumatatu, alichapisha video inayomuonyesha yeye na wengine kadhaa wakimuosha Morgan kama ishara ya kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Aliambatanisha video hiyo na ujumbe maalum kwa kijana huyo wa miaka 13 ambapo alionyesha fahari yake kubwa kuwa naye kama mwanawe.

"Angalia wewe Mtoto wangu Morgan Bahati, Ulitimiza miaka kumi na mitatu wiki chache zilizopita na ninajivunia jinsi ninavyofurahi kwa wewe kuniita Mama," aliandika chini ya video hiyo ambayo alipakia kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Mke huyo wa mwimbaji Bahati alisema ameona maendeleo na mabadiliko mengi kwa mwanawe na kumtakia mwongozo wa Mungu maishani.

"Nimekuona ukibadilika na kuwa Muungwana uliye leo na kitu ninachoweza kusema ni kwamba Mungu aendelee kukulinda na aniongoze mimi na Baba yako siku zote tuweze kukulea ili uwe toleo bora kwako," alisema.

Mama huyo wa watoto watatu pia alionyesha fahari yake kubwa kwa kumpa Morgan alichotaka kwa siku yake ya kuzaliwa.

Morgan alitimiza miaka 13 tarehe mnamo Desemba 22 mwaka jana,  siku ambayo babake Bahati alisherehekea kutimiza miaka 30.

Bahati alifichua kuwa anashiriki tarehe sawa ya kuzaliwa na mwanawe huyo kwa kuwa  ni maalum kwake na anamweka karibu na moyo wake.

"Ninashiriki tarehe sawa ya kuzaliwa na mwanangu @morgan_bahati kwa sababu yeye ni maalum sana kwangu na ako karibu na moyo wangu❤," Bahati alisema takriban kupitia Instagram takriban wiki tatu zilizopita.

Mtunzi huyo wa wimbo 'Mama'  alimchukua Morgan kuwa mtoto wake mwaka wa 2014 wakati alipoenda kutumbuiza katika nyumba ya  watoto yatima ya ABC ambapo alikulia pia baada ya mama yake kuaga dunia.

Baada ya Bahati kutumbuiza, Morgan alikataa kurejea katika kituo hicho cha watoto na akataka kwenda naye.

Huku akizungumzia matukio ya kipindi hicho mwaka jana, msanii huyo alisema alikuwa wakati huo hakuwa na uwezo mkubwa wa kifedha kumwezesha kuasili mtoto.

“Baada ya shoo mtoto  mdogoMorgan mwenye umri wa miaka 2 alilia kwenda na mimi nyumbani, ilikuwa ngumu kwangu kwa sababu nilikuwa bado natatizika kifedha.. Mbaya zaidi niliishi kwenye chumba kidogo na sikuwa na mtu wa kumlea mtoto kwa sababu nilkuwa nikiikaa peke yangu,'' alisema.

Morgan amekuwa akiishi na Bahati tangu wakati huo na mwimbaji huyo amekuwa akimtunza vizuri kama mtoto wake wa kuzaa.