"Niombeeni" Mr Seed ahuzunika baada ya kushindwa kutembea, kujiosha kufuatia ajali

"Siku 25 kwenye kitanda hiki, sijaweza kutembea au kujisafisha baada ya ajali. Hii inasikitisha," alisema.

Muhtasari

•Mr Seed alihusika katika ajali mbaya ya barabarani mwishoni mwa mwezi uliopita na amekuwa akiuguza majeraha nyumbani.

•"Endeleeni kumuombea Mr Seed. Nitaamka tena #NikoPoa," alisema.

awezwa na hisia wakati wa mazishi ya mpiga picha wake Ambrose Khan katika eneo la Igembe North mnamo Jumamosi, Mei 6, 2023.
Mr Seed awezwa na hisia wakati wa mazishi ya mpiga picha wake Ambrose Khan katika eneo la Igembe North mnamo Jumamosi, Mei 6, 2023.
Image: HISANI

Mwimbaji mashuhuri wa nyimbo za injili na za mapenzi Moses Tarus  Omondi almaarufu Mr Seed amewaomba mashabiki wake kumkumbuka katika sala zao huku akifichua kuwa anapambana na msongo wa mawazo.

Mr Seed alihusika katika ajali mbaya ya barabarani mwishoni mwa mwezi uliopita na amekuwa akiuguza majeraha nyumbani.

Katika taarifa yake  ya Jumanne, msanii huyo wa zamani wa EMB alisema kutoweza kufanya mambo ya msingi kama vile kutembea na kujiosha kwa siku 25 ambazo amekuwa akiuguza majeraha kitandani kumemsumbua sana.

"Siku 25 kwenye kitanda hiki, sijaweza kutembea au kujisafisha baada ya ajali. Hii inasikitisha," alisema kwenye Instagram.

Mwimbaji huyo aliambatanisha taarifa yake na emoji za uso wenye machozi kuashiria uchungu mwingi ndani yake.

"Endeleeni kumuombea Mr Seed. Nitaamka tena #NikoPoa," alisema.

Mwishoni mwa mwezi Aprili, Mr Seed alihusika katika ajali mbaya ya barabarani kwenye barabara ya Nanyuki-Nairobi.

Kulingana na mke wake Nimo Gachuiri, alikuwa kwenye gari na baadhi ya marafiki zake mnamo Aprili 29 wakielekea kuona ardhi fulani katika eneo Nanyuki wakati ajali ilitokea. Mmoja wao aliaga huku wengine wakijeruhiwa.

“Siamini kama  mume wangu yuko hai. Sijawahi patwa na wasiwasi kama huu maishani mwangu. Wasamaria wema walinisaidia na tulimkimbiza hospitalini. Nilikuwa nachukua video hizi kwa ajili ya wanafamilia,” Nimo alisema.

Nimo alisimulia kwamba gari ambalo mumewe alikuwa ndani lilikuwa mbele ya lile ambalo yeye alikuwa anasafiria na walipigwa na butwaa walipoona watu wamejumuika na kufika wakapata ni mumewe na wenzake wamepata ajali.

"Nakumbuka tu nilikimbia na kuwaona chini na kumwomba waamke. Sijui kama niwe na furaha kwamba baadhi ya marafiki walisalimika katika ajali hiyo kwa sababu pia siwezi kosa kulia kuwa baadhi walipoteza maisha,” Nimo alisema.

Nimo alisema alichokiona ni muujiza kwani mumewe alikuwa hai ingawa alikuwa na maumivu makali kutokana na majeraha aliyoyapata.

“Seed ako sawa hata ingawa ana maumivu kwenye nyonga. Ameagizwa kuwa kitandani kwa wiki mbili. Tuombeeni na pia zile familia za wale ambao kwa bahati mbaya walifariki,” Nimo aliandika.

Takriban wiki tatu zilizopita, Mr Seed alipambana na majeraha na kuhudhuria mazishi ya mpiga picha wake Ambrose Khan ambaye alifariki katika ajali hiyo,

Wakati wa maziko hayo, mwanamuziki huyo alionekana akihangaika kusimama na kutembea  alipoombwa kuwasalimia waombolezaji. Pia alionekana akilia kwenye eneo la kaburi la marehemu baada ya kuzikwa shambani mwao.

Badaye, aliwafahamisha mashabiki wake kuwa atachukua mapumziko kutoka kwenye mitandao ya kijamii kwa muda ambao haujawekwa wazi ili kuangazia afya yake ya mwili na ya kiakili.

"Ninatoka kwenye mitandao ya kijamii kwa muda, nahitaji kujishughulisha na afya yangu/akili yangu. Nitarudi hivi karibuni. Baraka. Nawapenda mashabiki wangu, tuonane hivi karibuni," alisema.