•Nyanyake Chira alikaribisha kikundi cha wanatiktok kwenye nyumba yake mpya ili kusherehekea kukamilika kwa ujenzi.
•Kama alivyoahidi, nyanyake Chira aliipa nyumba hiyo jina la mjukuu wake na jina ‘Chira Clan’ limeandikwa kwenye ukuta.
Siku ya Jumamosi, hafla ya kupendeza ilifanyika kuzindua rasmi nyumba mpya ya kisasa iliyojengwa kwa ajili ya nyanya wa marehemu Brian Chira.
Nyumba hiyo ambayo ilijengwa kwa kutumia fedha zilizochangwa na kundi la watumizi wa mtandao wa tiktok kufuatia kifo cha mwenzao Chira mapema mwaka huu ilikamilika hivi majuzi. Inakadiriwa kugharimu takriban Ksh6-8milioni na imejengwa katika eneo la Githunguri, Kaunti ya Kiambu.
Nyanyake Chira, Bi Esther Njeri, mnamo Jumamosi alikaribisha kikundi cha wanatiktok kwenye nyumba yake mpya ili kusherehekea kukamilika kwa jengo hilo na kulifungua rasmi kabla ya kuhamia ndani yake.
“Nashukuru tu kwa wema wenu, siwezi kuamini, huwa naomba Mungu aibariki TikTokers, endeleeni kuwasiliana nasi. Endeleeni kupiga simu zetu, nawapenda sana. Siamini mlichotufanyia.
Mungu awabariki. Endeleeni kunitembelea. Mnaweza kuona jinsi nilivyojenga nyumba kubwa. Tutaweka vyumba vya wageni ili muweze kututembelea hapa. Nyumba hiyo itaitwa Chira Clan," Bi Njeri alisema muda mfupi uliopita kwenye video iliyonaswa na Obidan Dela.
Kama alivyoahidi, nyanyake Chira aliipa nyumba hiyo jina la mjukuu wake na jina ‘Chira Clan’ limeandikwa kwenye ukuta.
Ujenzi wa nyumba hiyo ya mamilioni ulianza baada ya kifo cha Brian Chira mwezi Machi mwaka huu. Tiktokers waliamua kuchangisha fedha kwa ajili ya jengo hilo, katika jitihada za kutimiza ndoto ya marehemu Chira ya kumjengea nyanya yake nyumba.
Baada ya mazishi ya Chira mwezi Machi, Baba Talisha ambaye alisimamia miamala yote ya michango kwa ajili ya kufanikisha hafla hiyo alitoa maelezo jinsi michango hiyo iliyotumika. Michango ilikuwa imevuka shilingi za Kenya milioni 8.
Baba T alitoa taarifa kwenye kipindi cha moja kwa moja na pia akaonyesha nyaraka za maelezo ya jinsi michango yote kupitia M-Pesa na benki ilivyoratibiwa na kutumiwa, lakini pia kiasi cha pesa zilizosalia na kazi ya baada ya Chira kuzikwa .
Baba Talisha alieleza ni hela ngapi kutokana na michango hiyo ambazo zilitumika katika usafiri kutoka Nairobi kwenda Githunguri kwa nyanyake Chira alikozikwa, vyakula, maturubai miongoni mwa vitu vingine.
"KSh 498, 125. Ilitubidi kununua vyakula vingine. Hapo awali tulipanga bajeti ya watu 600 au 700, lakini wakati wa mazishi, tulilazimika kuongeza chakula zaidi. Tulilipa amana ya 105,000, na tulikuwa na nakisi ya 29,000, na tulilipa yote," Baba Talisha alisema.
Baba T pia alifichua kuwa kiasi kilichosalia ni KSh 7.2 milioni baada ya kulipakiasi walichokuwa wakidaiwa.
“Balance iko kwa benki ni KSh 7.2 milioni. Baada ya nimemaliza kulipa deni, nyanyake Chira amepewa taarifa kwamba kwa mwezi wa tano, anafaa kuwa kuhama huko, hivyo tunatakiwa tuwe na haraka,” Baba T alisema.