Nyota Ndogo aonyesha mimba yake nene, afichua mipango maalum ya wakwe zake kwa mtoto aliyebeba

Nyota Ndogo alikiri fahari yake kwa jinsi mtoto anayembeba ameendelea kukua vizuri tumboni mwake.

Muhtasari

•Nyota Ndogo aliposti video iliyoonyesha tumbo lake likiwa limechomoza huku kijusi kilicho ndani yake kikionekana kubisha.

•Alidai kuwa mtoto aliyembeba alifurahi baada ya kusikia kuwa wakwe zao watawatembelea hivi karibuni kutoka Denmark.

Image: INSTAGRAM// NYOTA NDOGO

Siku ya Jumapili, mwanamuziki mkongwe mzaliwa wa pwani Mwanaisha Abdalla almaarufu Nyota Ndogo aliwaonyesha mashabiki wake ujauzito wake mkubwa kwenye mitandao ya kijamii.

Mwimbaji huyo wa kibao ‘Watu na Viatu’ alishiriki video ambayo ilionyesha tumbo lake likiwa limechomoza sana huku kijusi kilicho ndani yake kikionekana kubisha.

Katika sehemu ya maelezo ya posti yake, mwimbaji huyo mkongwe alidai kwa utani kuwa mtoto aliyembeba alifurahi sana baada ya kusikia kuwa wakwe zao wazungu watawatembelea hivi karibuni kutoka Denmark.

"Kaskia familia nzima kutoka Denmark inakuja kwa ajili yake basi leo kacheza sana," Nyota Ndogo alisema kwenye Instagram.

Mama huyo wa watoto wawili ambaye kwa sasa ameolewa na mwanaume mzungu kutoka Denmark, Henning Neilsen pia alieleza fahari yake kwa jinsi mtoto anayembeba ameendelea kukua vizuri  tumboni mwake.

Mwimbaji Nyota Ndogo alitangaza habari za ujauzito wa ambaye atakuwa mtoto wake wa tatu mapema mwezi Septemba  kutumia picha ambayo  ilimuonyesha akiwa ameshika tumbo lake lililoonekana kuchomoza.

Baadaye, mama huyo wa watoto wawili hata hivyo aliweka wazi kuwa mume wake, Henning Neilsen amemuonya dhidi ya kuzungumza mengi kuhusu ujauzito wake na vyombo vya habari au watu wengine wa nje.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 42 ambaye kwa sasa anaendesha mkahawa wake katika eneo la VoI alisema ameruhusiwa tu kujizungumzia yeye na muziki wake na sio ujauzito hadi atakapojifungua.

“Asanteni kwa hongera zenu, lakini media mtanisamehe mume wangu amesema hataki kuona kwenye kituo chochote cha radio TV ama polisi nikiongelea hali yangu. Kwa hiyo endapo nitatoa interview iwe ya mimi na mziki wangu na sio ujauzito wangu, ama nisitoe mpaka nijifungue,” Nyota Ndogo alisema.

Baadaye mwezi huo, Nyota Ndogo alifichua kwamba mume wake mzungu alikuwa amemnunulia shamba lenye thamani ya shilingi milioni tatu ambapo anakusudia kujenga hoteli kubwa zaidi ya anayoendesha kwa sasa.

"Nimekua nikiona jumbe nyingi kuhusu hoteli yangu kua niko kibandani mara hapa sio hadhi yako na wengine hata kunifanani na kina shishi kinaa @esha.s.buheti ambao ndio watu ninao waangali na kufata nyayo zao. Lakini ni miaka sita sasa pale hotelini na sijakua na haraka yakufanya kitu ama kujipa presha kwaku wenzangu wapo vizuri hapana, naendaga na time, na time ndio saa," alisema Nyota Ndogo.

Mwanamuziki huyo mkongwe alisema mumewe alimzawadia shamba hilo na kuliandikisha kwa jina lake.

"NAKUNIAMBIA ANDIKA JINA LAKO HIO NI YAKO KWAKUA UNANIPENDA KWELI. PLOT YENYEWE IMENUNULIWA MILIONI TATU NA IPO VOI. Sasa inshallah tujenge mkahawa wetu pendwa.kila kitu na mna wake.wakati wa MUNGU.ndio sawa." alisema.