Omosh aapa kumuombea mpwa wake Baha kukabiliana na uraibu wa kamari, amshauri jinsi ya kuacha

"Kila maombi ninayofanya katika maisha yangu, kutakuwa na mstari wa Baha kupambana na uraibu huo," Omosh alisema.

Muhtasari

•Omosh amemshauri mpwa wake Tyler Mbaya kumgeukia Mungu ili amsaidie kupambana na uraibu wa kucheza kamari ambao alidaiwa kuwa nao mapema mwaka huu.

•Omosh alifunguka kuhusu jinsi uraibu wa kucheza kamari ulivyomfanya akumbwe na matatizo ya kifedha katika siku zake za ujana.

mpwa wake Tyler Mbaya jinsi ya kupambana na uraibu wa Kamari.
Omosh amemshauri mpwa wake Tyler Mbaya jinsi ya kupambana na uraibu wa Kamari.
Image: INSTAGRAM

Aliyekuwa muigizaji wa Tahidi High, Joseph Kinuthia almaarufu Omosh Kizangila amemshauri mpwa wake Tyler Mbaya kumgeukia Mungu ili amsaidie kupambana na uraibu wa kucheza kamari ambao alidaiwa kuwa nao mapema mwaka huu.

Katika mahojiano na Mungai Eve, Omosh ambaye anadai kuwa sasa ameokoka alibainisha kuwa maombi huwasaidia watu kupambana na uraibu wa aina yoyote ambao wanaweza kuwa nao.

Alimfahamisha muigizaji huyo wa zamani wa Machachari kwamba shetani anaweza kumvuta nyuma katika vita vyake dhidi ya uraibu na kumbainishia kuwa Mungu pekee anaweza kumsaidia kupambana nao.

“Kitu pekee ambacho kinaweza kumsaidia, mimi kama mjomba wake, aende kwa Mungu katika maombi. Unaweza pata kuna kitu kimoja anajaribu kutoka lakini inamshinda. Huyo ni Shetani anakuvuta nyuma. Shetani atakuvuta nyuma kila mara,” Omosh alisema.

Aliongeza, “Yeyote anapambana na uraibu fulani, shetani hatakangi utoke kwa uraibu huo. Lakini ukisisitiza katika maombi, Mungu anaweza kushuka juu ya uraibu huo na utaushinda.”

Muigizaji huyo wa zamani wa Tahidi High aliahidi pia kumwombea mpwa huyo wake kila siku hadi atakapofanikiwa kupambana na uraibu wa kucheza kamari.

Aidha, alikiri kuwa hapo awali hakufahamu kuhusu tatizo ambalo Tyler amekuwa nalo lakini akaahidi sasa kumtafuta na kumsaidia kupambana nalo.

Nitaendelea kumuombea mpwa wangu na siku moja najua, yeye mwenyewe atasema imeisha. Kila maombi ninayofanya katika maisha yangu, kutakuwa na mstari wa Baha kupambana na uraibu huo.

Nitatafuta muda tuende tubonge. Mtu kama huyo hutaka watu kumuonyesha upendo. Bado ni wetu, bado mimi nitabaki kuwa mjomba wake na upendo wote. Huyo mtoi nampenda na najua hiyo kitu itaisha,” alisema.

Wakati huo huo, Omosh alishangaa kwani uraibu wa kucheza kamari unaweza kuwa tatizo la familia huku akifichua kwamba pia yeye alipambana na uraibu huo katika siku za nyuma.

Muigizaji huyo alifunguka kuhusu jinsi uraibu wa kucheza kamari ulivyomfanya akumbwe na matatizo ya kifedha katika siku zake za ujana ambapo angetumia mshahara wake wote kwenye michezo.

‘Mimi nikiwa mdogo nilikuwa na uraibu wa kamari. Kwani ni shida ya kifamilia inayotuandama? Kuna Krismasi nilikula huku nimevaa slippers. Siku ya Krismasi nilikuwa na slippers. Nilikuwa nishawekea kamari ikachukua za ndula, za watoi za nguo zikasosiwa. Nakumbuka vizuri sana nikitoka Machakos Country Bus nikienda nyumbani. Nilikuwa nafanya kazi wakati huo, nilikuwa naokota takataka. Nilikuwa napata mshahara wangu mbio mbio naenda kamari nawekelea,” alisimulia.

Muigizaji huyo wa zamani wa Tahidi High ambaye hivi karibuni alikuwa akipambana na uraibu wa pombe alishauri mtu yeyote anayepitia uraibu wa jambo lolote kumweleza Mungu matatizo yake na kumwacha awasaidie kukabiliana nayo.