• Diamond alishare video nzuri ya mpenzi huyo wake wa zamani akiufurahia na kuupigia debe wimbo wake mpya na Jay Melody na Mr Blue, 'Mapoz.'
•Shakib alionyesha shukrani zake baada ya Diamond kusifia mapenzi mazito ambayo amekuwa akimpa mzazi mwenzake, Zari Hassan.
Mfanyibiashara wa Uganda, Shakib Cham Lutaaya alionyesha shukrani zake baada ya staa wa bongofleva Diamond Platnumz kusifia mapenzi mazito ambayo amekuwa akimpa mzazi mwenzake, mwanasosholaiti Zari Hassan.
Katika posti ya hivi punde kwenye ukurasa wake wa Instagram, Diamond alishare video nzuri ya mpenzi huyo wake wa zamani akiufurahia na kuupigia debe wimbo wake mpya na Jay Melody na Mr Blue, 'Mapoz.'
Bosi huyo wa WCB alitumia nafasi hiyo kufichua jinsi mzazi mwenzake huyo alivyoridhishwa na mapenzi anayoyapata kutoka kwa mpenzi wake wa sasa, Shakib Lutaaya.
“Mama Tee @zarithebosslady anakwambia mapenzi anayopata @shakib_cham ni kilo 150. Ndivyo anavyopata raha hata iweje. The boss lady, mzungu wa roho,” aliandika Diamond chini ya video ya Zari Hassan aliyoiweka Jumapili. .
Kwa kweli, wengi wangepokea vibaya ikiwa mpenzi wa zamani wa mke wao angemposti kwenye ukurasa wake na kuambatanisha na nukuu kama ile aliyotumia Diamond. Lakini haikuwa hivyo kwa Shakib, badala yake alionekana kujivunia kile ambacho mzazi mwenza wa mkewe alikuwa amechapisha.
Katika jibu lake kwa staa huyo wa Bongo, mfanyabiashara huyo wa Uganda mwenye umri wa miaka 31 alionyesha shukrani na kumtambua kama shemeji yake.
“Powa Shemej @diamondplatnumz,” Shakib alimjibu Diamond.
Hiki ni kidokezo wazi kuwa wanaume hao wawili maalum katika maisha ya Zari Hassan hawana uhasama wowote na badala yake wana uhusiano mzuri.
Hii hata hivyo si mara ya kwanza kwa Diamond na Shakib kuonyesha wazi uhusiano mzuri kati yao. Mwezi Oktoba mwaka jana, video na picha zao wakiwa pamoja zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii na walipata sifa kwa ukomavu walioonyesha.
Akizungumzia mkutano huo, Zari alisema kuwa mzazi mwenzake huyo alitaka kuonana na mtu ambaye anatumia muda mwingi na watoto wake, ndiyo maana ilimlazimu (Zari) kupanga wakutane.
Mama huyo wa watoto watano alitaja kwamba wanaume hao wawili walikuwa wamekomaa kuhusu mkutano huo na ndiyo sababu ilikuwa rahisi kwake.
"Nadhani, ni sisi wanawake ambao tunapenda kuvuta kamba, lakini kwa wanaume wawili, walikuwa wazuri sana," alisema.
“Kipindi cha nyuma, nakumbuka nilikaa na Diamond na nilipomwambia kuwa nimeolewa alisema anataka kuonana na mtu wangu," Zari alisema.
Zari alisema Diamond alitaka "kujua aina ya mtu ambaye alikuwa akitumia muda mwingi na watoto wake kuliko yeye."
"Kisha nikazungumza na Shakib kuhusu hilo... nikamuuliza kama alikuwa anataka na akasema ndio. Mwishowe, lilikuwa jambo rahisi zaidi kufanya."
"Alikiri kwamba hayuko tena katika maisha ya watoto na akasema alifurahi kwamba (Shakib) alikuwa mtu mkarimu na mzuri. Hivi sasa ni marafiki wazuri," aliongeza.