logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Sababu za Diamond kufanikiwa kuliko wasanii wengine zafichuliwa

Mkubwa Fella amedai itachukua miaka mingi kupata msanii mwingine kama Diamond au wa kuridhi nafasi yake.

image
na Samuel Maina

Burudani24 October 2022 - 12:10

Muhtasari


  • •Mkubwa Fella alibainisha kuwa Diamond Platnumz ameweka kiwango cha juu sana kwa wasanii wengine.
  • •Fella alisema usupastaa wa Diamond haujamfanya kuwa na ujeuri au kumfanya adharau waliomlea.

Mkubwa Fella, mmoja wa mameneja wa WCB amedai kwamba itachukua miaka mingi kupata msanii mwingine kama Diamond Platnumz au wa kuridhi nafasi yake kwenye Tasnia ya Muziki wa Bongo.

Katika mahojiano na Bongo 5, Fella alibainisha kuwa Diamond ameweka kiwango cha juu sana kwa wasanii wengine.

Alidokeza kuwa yeye na mameneja wenzake, Babu Tale na Salaam SK wamefanikisha mafanikio makubwa ya Diamond.

"Kama bado niko mimi, Tale na Salaam hawezi kutokea msanii mwingine kumpita Naseeb. Sisi Mungu atuchukue ama mimi niamue kupumzika, Tale aje kupumzika ndio wataanza kucharuka wengine," alisema.

Fella alifichua kwamba ujasiri wao katika kuwekeza umechangia mafanikio makubwa ya lebo ya Diamond na WCB kwa ujumla.

Alimpongeza Diamond kwa uaminifu wake na heshima yake kubwa. Alibainisha kuwa licha ya staa huyo wa Bongo kuwa Bilionea bado anawaheshimu wale ambao walimsaidia alipokuwa akipanda ngazi.

"Hajawahi kutudharau hadi siku moja. Anajua sisi ni watu ambao tulimtoa pale chini mpaka leo yuko pale juu," alisema.

Fella alisema kiwango cha usupastaa cha Diamond hakijamfanya kuwa na ujeuri au kumfanya adharau waliomlea.

Pia aliwakosoa wasanii ambao walijitenga na walezi wao njiani na kusema hatua hiyo iliwagharimu taaluma zao.

"Kuna wengi ambao tulianza nao lakini  baada ya kupata laki mbili, laki tatu wakaanza kuwa wajeuri. Wengine baada ya kupata laki nane, laki sita wakakimbia, kumbe kukimbia kule ikawa unajipotezea mwenyewe riziki yako. Saa zingine Mungu alitaka mkae pamoja mfanikiwe," alisema Fella.

Fella alifichua kuwa bosi huyo wa WCB anamshukuru sana Mungu kwa mafanikio yake na ndiyo maana amekuwa akiomba mara kwa mara.

"Alikuwa anamuomba Mungu ampe hela, sasa yeye ana hela. Sasa yeye ana haki ya kumrudishia shukrani ndio maana anafanya ibada sasa. Ibada zake ni za shukrani"

Meneja huyo alibainisha kuwa anajivunia kazi ambayo amemfanyia Diamond na matunda yaliyozaliwa kutokana na hilo.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved