Sauti Sol kutumbuiza pamoja mara ya mwisho kwenye Yetu Festival na Sol Fest

Walisisitiza kwamba urafiki wao na maono ya pamoja yataendelea kuwa nguvu ya kuendesha miradi yao ya baadaye.

Muhtasari

•Sauti Sol wametangaza kuwa watapumzika ya kufanya kazi pamoja kama kikundi kwa muda usiojulikana.

•Walisema kuwa miaka zaidi ya 20 ambayo wamekuwa pamoja imekuwa safari nzuri kwao kama wasanii na marafiki.

Sauti Sol
Image: HISANI

Tamasha lijalo la Stanbic Yetu Festival na Sol Fest huenda zikawa mara za mwisho ambapo mashabiki wa bendi maarufu ya Kenya, Sauti Sol kuwaona wakitumbuiza pamoja.

Siku ya Jumamosi, bendi hiyo inayojumuisha wasanii wanne ilitangaza kuwa watapumzika kufanya kazi pamoja kama kikundi kwa muda usiojulikana.

Katika taarifa kwa mashabiki wao, wanabendi hao walisema hii itaanza baada ya kukamilika kwa ratiba yao ya ziara ya dunia ambapo wameratibiwa kutumbuiza katika mataifa mbalimbali barani Ulaya na Amerika.

"Ziara inayokuja katika nchi za Marekani, Ulaya na Kanada ni fursa kwa mashabiki kufurahia ubabe wa Sauti Sol kwa mara ya mwisho kabla bendi haijapumzika kwa muda kutoka kwa miradi ya kikundi. Kila shoo itachangiwa na hisia ya upendo wa dhati na shukrani huku kikundi kikitoa vibao vyao visivyoishiwa na wakati na vipendwa vya mashabiki ambavyo vimeacha alama isiyoweza kufutika kwenye kumbukumbu zetu za pamoja," walisema.

Waliongeza, "Wakati mapumziko ya muda usiojulikana yakionyesha mwisho wa ukurasa maalum, pia inawakilisha mwanzo mpya wa Sauti Sol.

Bendi hiyo ilisisitiza kwamba urafiki wao na maono ya pamoja yataendelea kuwa nguvu ya kuendesha miradi yao ya baadaye.

Walisema kuwa miaka zaidi ya 20 ambayo wamekuwa pamoja imekuwa safari nzuri kwao kama wasanii na marafiki.

"Tumejawa na shukrani kwa upendo na usaidizi ambao tumepokea kwa miaka yote. Wakati tunachukua mapumziko haya kutekeleza miradi yetu ya kibinafsi na ya pamoja, tunasalia kujitolea kwa urafiki wetu na biashara zetu za pamoja. Uhusiano kati yetu hauwezi kuvunjika na sisi tuna shauku kwa yale yajayo."

Tangazo hilo linakuja kabla ya shoo yao iliyoratibiwa katika Tamasha la Stanbic Yetu jijini Nairobi mnamo Juni 10.

Bendi hiyo ya wanamuziki wanne itatumbuiza kwenye tamasha la Yetu Festival mnamo Juni 10 na baadaye kwenye Sol Fest mwezi Agosti.