“Shetani alikuwa kazini” Diana Marua azungumzia tukio la kutisha lililompata na watoto wake Thika Road

Diana alifichua kwamba alikuwa na watoto wake Morgan, Mueni, Heaven, Majesty, na Josh wakati tukio hilo lilipotokea.

Muhtasari

•Diana Marua ametoa taarifa akisimulia tukio la kutisha alilopitia akiwa na watoto wake kwenye Barabara ya Thika siku ya Jumapili usiku.

•Alifunguka alivyojawa na hofu baada ya kugundua tairi ya gari lake ilikuwa imepasuka kabla ya hatimaye kuweza kupunguza mwendo na kusimama.

Image: INSTAGRAM// DIANA MARUA

Mtayarishaji wa maudhui maarufu wa Kenya Diana Marua ametoa taarifa akisimulia tukio la kutisha alilopitia akiwa na watoto wake kwenye Barabara ya Thika siku ya Jumapili usiku.

Katika taarifa ya Jumatatu jioni, mke huyo wa mwimbaji Kelvin Bahati alifichua kwamba alikuwa na watoto wake Morgan Bahati, Mueni Bahati, Heaven Bahati, Majesty Bahati na Josh wakati tukio hilo lilipotokea.

Walikuwa wakielekea nyumbani kutoka kujiburudisha kwenye sehemu ya burudani wakati gari lake aina ya Range Rover Vogue  lilipopasuka tairi na kuanza kuyumba na kukosa kudhibitika.

"Siku iliyoanza kama nzuri na watoto Morgan Bahati, Mueni Bahati,Heaven Bahati, Majesty Bahati na Josh iligeuka kuwa Ndoto yangu mbaya zaidi! Shetani alikuwa kazini lakini Malaika wa Mungu  walikuwepo, Kuheshimu Agizo lao la kuwatunza Mabinti & Wana wa Mungu 😭🙏🏼,” Diana Marua aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Aliongeza, "Tulitoka tumetoka nje,  tukiimba nyimbo za kurudi nyumbani, tukipeana motisha juu ya mvua hii kubwa ambayo imekuwa kawaida. Sikujua, tairi lilipasuka na lilikuwa limechakaa hadi kwenye ream. Gari letu lilikuwa likiyumba bila udhibiti.”

Mama huyo wa watoto watatu alifichua jinsi alivyojawa na hofu baada ya kugundua tairi ya gari lake ilikuwa imepasuka kabla ya hatimaye kuweza kupunguza mwendo na kusimama.

Kufuatia tukio hilo, mtayarishaji huyo wa maudhui alitoa shukrani zake kwa Mungu kwa kumlinda yeye na familia yake na mumewe kwa kuwasaidia baada ya tukio hilo.

“Niliingiwa na hofu, mshtuko na kuchanganyikiwa! Nilifanikiwa kupunguza mwendo na kusimama kando ya barabara tu kwa ajali mbaya kutokea dakika tano baadaye, mita chache kutoka kwa gari letu. Mume wangu @bahatikenya alikuja kwa wakati na ninachoweza kusema ni ASANTE MUNGU! HUWA HAFELI🙏🏼🙏🏼🙏🏼 ,” Diana alisema.

Jumapili usiku, Bahati alilazimika kukimbia kumsaidia mkewe Diana Marua baada ya gari lake kupata tatizo na kukwama kwenye Barabara ya Thika.

Bahati alichapisha video ya tukio hilo kwenye ukurasa wake wa Instagram akionyesha jinsi gurudumu la mbele la gari la Diana aina ya Range Rover Vogue lilivyopasuka na kumfanya asimame kwenye barabara.

Alimshukuru Mungu kwa kumlinda mkewe na watoto waliokuwa naye wakati wa tukio hilo huku akibainisha kuwa wote walikuwa wameingiwa na hofu.

"Mke wangu na watoto bado wako chini ya shambulio la hofu.. Hiki ndicho kilichowapata kwenye barbara ya Thika Super Highway.. Mungu ni mkubwa," Bahati alisema chini ya video aliyochapisha.

Katika video hiyo, mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili alisikika akielezea kisa hicho na pia kumshauri mke wake kile ambacho alipaswa kufanya baada ya tukio kutokea.

“Niko hapa kwenye Barabara ya Thika, Mvua inanyesha. Niko hapa kumwokoa Diana. Diana amekwama na watoto kwa Thika Super Highway,” Bahati alieleza.

Huku akimgeukia mkewe Diana, mwimbaji huyo alimwambia, “Sasa, kitu utafanya, utatoa watoto. Lakini babe, mtu akibondwa huenda pande ile nyingine. Mahali mko ni hatari, yaani ni Mungu amewasaidia. Ona watu wameegesha nyuma yenu. Mimi nilidhani ni nyinyi mmepata ajali.”

Diana alieleza kuwa kufikia wakati alipogundua tairi lake lilikuwa limepasuka, tayari ilikuwa kuchelewa na gari halikuweza kusonga tena.