“Simu yako siachi kushika!” Fahyma amuonya mumewe Rayvanny huku akimuombea dua maalum

"Tusameheane pindi tunapokosana, binafsi naomba tu univumilie maana nina mdomo sana," Fahyma alimwambia mumewe.

Muhtasari

•Fahyma alitaka msamaha kuwa sehemu ya mahusiano yao na akamwomba mwimbaji huyo awe na subira naye kila wakati.

"Jambo lingine mume wangu, simu yako kushika siachi hilo ulijue! Nakupenda sana kuliko chochote hapa duniani,” Fahyma alisema.

Image: INSTAGRAM// FAHYMA

Staa wa Bongo, Raymond Mwakyusa almaarufu Rayvanny anasherehekea siku yake ya kuzaliwa leo, Septemba 22. 

Mashabiki, wanamitandao, wasanii wenzake na watu wengine wa karibu katika maisha yake wameendelea kumsherehekea bosi huyo wa Next Level Music kwa meseji nzuri akiadhimisha siku yake ya kuzaliwa. 

Miongoni mwa watu waliomsherehekea mwanamuziki huyo ni mpenzi wake, Fahyma ambaye amemwandikia ujumbe mtamu wa mahaba na kumhakikishia kuhusu mapenzi yake mazito kwake.

“Heri ya siku ya kuzaliwa mume wangu pekee @rayvanny. Nakupenda sana kila siku za maisha yangu,” Fahyma alimwandikia mumewe.

Mama huyo wa mtoto mmoja aliendelea kufanya maombi maalum kwa ajili ya Rayvanny ambapo alimwomba Mungu ammiminie mvua ya mafanikio mengi. 

Wakati huo huo, mrembo huyo alitaka msamaha kuwa sehemu ya mahusiano yao na akamwomba mwimbaji huyo awe na subira naye kila wakati.

“Namuomba MUNGU atujaalie na atutimizie kila hitaji la mioyo yetu. Nakuombea mafanikio mengi katika kazi zako mume wangu, Nakupenda, nakuthamini na kuheshimu pia. Tusameheane pindi tunapokosana, binafsi naomba tu univumilie maana nina mdomo sana. Na jambo lingine mume wangu, simu yako kushika siachi hilo ulijue! Nakupenda sana kuliko chochote hapa duniani,” Fahyma aliandika.

Mwanamitindo huyo na mzazi mwenzake, Rayvanny wamekuwa wakionyesha mapenzi mazito baina yao tangu warudiane mapema mwaka huu baada ya awali kutengana takriban miaka mitatu iliyopita.

Mwezi Aprili, Rayvanny alidhihirisha mapenzi yake kwa mzazi huyo mwenzake kwa kuchorwa jina lake kwenye kifundo cha mkono wake.

"Fahyma...❤," ilisomeka tattoo mpya ya mwimbaji huyo.

Bosi huyo wa Next Level Music alionyesha video yake akichorwa katika duka moja la tattoo jijini Arusha, Tanzania na akaweka wazi alichukua hatua hiyo kutokana na mapenzi yake makubwa kwa mzazi huyo mwenzake.

Alisema, licha ya kuwa ni chungu, alilazimika kufanya hivyo kutokana na athari kubwa ya Fahyma katika maisha yake.

"Inauma sana ila nimefanya hivi kwa ajili yako Fahvanny," alisema kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram.

Aliongeza, "Umekuwa mwanamke wa tofauti kwangu, nakuheshimu."

Alibainisha kwamba iwapo watu wangeelewa mapenzi yake kwa mwanamitindo huyo basi wangeelewa hatua hiyo yake.

"Hata ungekuwa wewe ungechora tu," alisema.