"Singejua nilichopangiwa!" DJ Fatxo afichua sababu ya kutohudhuria mazishi ya Jeff Mwathi

Singeandika kwenye kurasa zangu za mitandao ya kijamii kwa sababu yaliyokuwa yakisemekana sio kweli," alisema.

Muhtasari

•DJ Fatxo alisema aliwafahamisha wanafamilia wa marehemu kuhusu yaliyotokea baada ya kupiga ripoti katika kituo cha polisi.

•Alisema alikuwa tayari kusaidia familia katika mazishi lakini hakuweza kufanya hivyo kutokana na kutokuwa na mawasiliano mazuri

Mwimbaji DJ Fatxo na marehemu Jeff Mwathi
Image: HISANI

Mwimbaji wa Mugithi ambaye amekuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii katika kipindi cha takriban wiki moja iliyopita, Lawrence Njuguna almaarufu DJ Fatxo, amedai kwamba alijaribu sana bila mafanikio kuwasiliana na familia ya marehemu Jeff Mwathi ili kushirikiana nao katika mazishi ya mpendwa wao.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumapili, DJ Fatxo ambaye amekuwa akiangaziwa sana katika siku za hivi majuzi baada ya kijana huyo mwenye umri wa miaka 23 kuaga dunia akiwa nyumbani kwake alisema kwamba yeye ndiye alifichua habari za kifo cha Jeff kwa familia yake kwa njia ya simu.

Alisema aliwafahamisha wanafamilia wa marehemu kuhusu yaliyotokea baada ya kupiga ripoti katika kituo cha polisi.

"Kwa hakika niliwasiliana nao na kuwaambia ninaweza kuwasaidia wazike mtoto na tushirikiane nao kwa sababu ni kitu ambacho kilinihuzunisha hata mimi," alisema.

Mwimbaji huyo mzaliwa wa Nyandarua alisema kwa bahati mbaya hakukuwa na mawasiliano mazuri kati yake na familia ya Mwathi. Alisema alipiga simu zaidi ya mara nane katika juhudi za kuwasiliana na familia hiyo.

Baada ya kushindwa kuwa na maelewano na familia ya marehemu, Fatxo anasema alimwomba mama yake amsaidie.

"Nilimuomba mamangu apigie mwanafamilia mmoja awaombe tushirikiane nao kwa sababu hii ni kitu mpya kwangu. Hakuna jinsi ningepoteza rafiki nikose kumwomboleza. Labda Mama Jeff hakufikishiwa ripoti, labda hakuambiwa nataka tupatane. Lakini tuliwatafuta," alisema.

DJ Fatxo alisema alikuwa tayari kusaidia familia katika mazishi lakini hakuweza kufanya hivyo kutokana na kutokuwa na mawasiliano mazuri.

Pia aliweka wazi kuwa hangeweza kuhudhuria mazishi ya Jeff nyumbani kwao katika Kaunti ya Nakuru kwani hakujua ambacho kingetokea.

"Wakati mawasiliano yalikosekana, kusema kweli hata mazishi singeenda kwa sababu sijui nilichapangiwa. Singechapishwa kwenye kurasa zangu za mitandao ya kijamii kwa sababu yaliyokuwa yakisemekana sio kweli," alisema.

Mwanamuziki huyo alisema kufuatia hayo alichagua kusalia kimya na kuwaacha wapelelezi wafanye kazi yao.

Alieleza imani yake kwa timu mpya ya uchunguzi ya DCI akisema kwamba pia yeye anahitaji majibu kuhusu kilichotokea.