"Siwezi bila wewe, nathamini unachonifanyia!" Guardian Angel akiri kwa mke wake Esther Musila

"Kuna watu naweza kufanya bila wao, lakini wewe si mmoja wao,"Guardian Angel alimwambia mkewe.

Muhtasari

•Guardian Angel alibainisha kuwa Bi Esther Musila amekuwa akimuunga mkono sana maishani na kitaaluma.

•"Ninathamini sana kile unachonifanyia katika taaluma yangu ya muziki, tasnia ya injili. Na kwangu kama mwanadamu na mume," Guardian Angel alimwambia mkewe.

Guardian Angel wa Esther Musila
Image: HISANI

Mwimbaji wa nyimbo za injili Peter Omwaka almaarufu Guardian Angel ametoa shukrani za dhati kwa mke wake Esther Musila kwa sapoti kubwa ambayo ameendelea kumpatia katika taaluma yake ya muziki.

Katika video ya pamoja ambayo walishiriki siku ya Jumatano, mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 33 alibainisha kuwa Bi Esther Musila amekuwa akimuunga mkono sana maishani na kitaaluma.

Alikiri kuwa mke huyo wake mwenye umri wa miaka 53 amekuwa baraka kwake kiasi kwamba hawezi bila yeye.

"Asante kwa kuniunga mkono kila wakati. Msaada wako ni kitu ambacho siwezi kufanya bila," Guardian Angel alisema.

Aliongeza, "Kuna watu naweza kufanya bila wao, lakini wewe si mmoja wao. Ninathamini sana kile unachonifanyia katika taaluma yangu ya muziki, tasnia ya injili. Na kwangu kama mwanadamu na mume."

Wanandoa hao walitengeneza video hiyo maalum kwa ajili ya kuwashukuru wote waliochangia mafanikio ya wimbo mpya wa Guardian Angel na Rose Muhando, 'Gharama.'  Walitoa shukrani kwa mwimbaji huyo wa injili kutoka Tanzania kwa ushirikiano mzuri katika kutengeza wimbo huo na mashabiki kwa kuendelea kuutazama, kuusikiliza na kushabikia kibao hicho ambacho kiliachiwa mwezi uliopita.

Mwezi ambao ulipita, Bi Esther Musila alifichua kwamba aliombea muungano wake na mume wake Guardian Angel.

Akizungumza kwenye video, alifichua kuwa takriban miaka minne iliyopita, aliomba  kumsihi Mungu abadilishe maisha yake.

"Niliomba kwamba wakati nitafikisha miaka 50 mwaka wa 2020, Mungu abadilishe maisha yangu kabisa," Bi Musila alisema.

Mhasibu huyo alisema aliendelea kusali na kumwomba Mungu ampatie maana katika maisha yake. Alidokeza kuwa Mungu alijibu maombi miezi michache baadaye kwa kumletea mumewe Guardian Angel maishani.

“Mume wangu Peter Omwaka, namshukuru Mungu kwa ajili yako, namshukuru Mungu kwa kukuleta katika maisha yangu, kwa kukutumia kubadilisha maisha yangu, kwa kunionyesha upendo na unyenyekevu na kuyafanya maisha yangu kuwa mazuri,” alisema.

Musila alisema hayo akiadhimisha miaka mitatu tangu alipokutana na Guardian Angel siku ya Jumatatu, Machi 13, 2023.  Alisema tarehe 13 mwezi Machi daima itasalia kuwa maalum na ya maana kwake.

Wakati huo, Guardian Angel kwa upande aliweka wazi kuwa alimpenda mkewe punde baada ya kukutana naye. Katika taarifa yake, Angel alisema alipomwangalia Bi Musila aliona sifa zote anazohitaji kwa mke ndani yake.

"13/3/2020 ulinitazama ukaona supastaa. Hamu yako ilikuwa kuniona nikiwa vile ulivyoniona. Nilikutazama na kuona kila nilichotaka kwa mwanamke. Miaka mitatu baadaye sisi sote tuna kile tulichotaka," alisema.

Guardian Angel alimtaja mama huyo wa watoto watatu wakubwa kama mke mzuri na kukiri mapenzi makubwa kwake.