Stevo, mkewe wajawa bashasha baada ya mbunge Salasya kuwapa makazi ya heshima

Mbunge huyo alisema mkewe Stivo Simple Boy alimthibitishia kuwa nyumba hiyo ni sawa kwao.

Muhtasari

•Peter Salasya mnamo Jumanne alitimiza ahadi yake kwa mwimbaji Stivo Simple Boy ya kumpatia makazi ya heshima.

•Salasya alisema kuwa yuko tayari kumsaidia Stivo Simple Boy iwapo atafikiria kujitosa katika kazi zingine za kutengeneza pesa mbali na muziki.

Stivo Simple Boy na mbunge Peter Salasya
Image: TWITTER// PETER SALASYA

Mbunge wa eneo la Mumia East, Peter Salasya mnamo Jumanne alitimiza ahadi yake kwa mwimbaji Stevo Simple Boy ya kumpatia makazi ya heshima.

Mwanasiasa huyo kijana aliwapeleka Stevo na mke wake Grace Atieno hadi kwenye nyumba aliyowatafutia jijini Nairobi na kuthibitisha kwamba tayari alikuwa amemaliza kuilipia kodi.

Akizungumza na mwanahabari Presenter Ali ambaye alikuwa ameandamana na watatu hao kwenye ziara ya nyumba hiyo, Salasya alisema kuwa mke wa mwimbaji huyo kutoka Kibra alimthibitishia kuwa nyumba hiyo ni sawa kwao.

“Nilimuuliza mke wake ‘umependa hiyo place?’.. Bibi ndiye huwa anaamua. Alisema iko juu. Nikasema kama ashasema iko juu, iko sawa nikalipa. Kila kitu kiko sawa,” Salasya alisema.

Mbunge huyo wa muhula wa kwanza alithibitisha kuwa atamrudisha Bi Atieno shuleni kwa kozi fupi ya masuala ya urembo ili awe na ujuzi utakaomsaidia kukidhi mahitaji yake na kusaidia familia yao ndogo.

“Nitamlipia shule ili aweze kujikimu. Pia nitamfungulia duka la nguo ili aweze kujisimamia ili bwana akienda shoo akipata ama asipopata kwa nyumba bibi atakuwa sawa. Wawe wanasaidiana,” Salasya alisema.

Aidha, Salasya alisema kuwa yuko tayari kumsaidia Stivo Simple Boy iwapo atafikiria kujitosa katika kazi zingine za kutengeneza pesa mbali na muziki.

"Pia nilisema wale ambao waliahidi kumjengea kama hawatafanya hivyo ndani ya siku 15 zijazo nitaenda Oyugis nimtengezee nyumba huko alafu aanze hapo," alisema mbunge huyo.

Mkewe Stevo, Bi Atieno alimshukuru mwanasiasa huyo kijana ambaye pia aliahidi kuwapa shilingi elfu 30 ili kununua baadhi ya vitu vya nyumbani.

Rapa Stivo pia alimshukuru mbunge huyo na kuahidi kufanya kazi pamoja naye.

Mbunge Salasya alisema kuwa kesi ya Stevo Simple Boy ilimgusa kwani aliiona ni ya kweli na ilimkumbusha nafasi aliyokuwa nayo kabla ya kuwa mbunge mwaka jana.

Salasya alikutana na msanii huyo aliyekabiliwa na misukosuko mingi kwenye safari yake ya muziki siku chache zilizopita amba aliahidi kumhamisha.

Alikuwa ameomba kukutanishwa na msanii huyo kutoka Kibera baada ya hadithi yake kuenezwa kuanzia wiki jana jinsi amekuwa akipitia maisha magumu hadi kulala njaa licha ya kuwa na jina kubwa kwenye Sanaa.