Tunaomba sana tupate mtoto, ni ndoto yangu mwakani- Mpenziwe Wema Sepetu, Whozu afunguka

Mwimbaji huyo alisema ni hamu ya mke wake Wema Sepetu kupata mtoto wa kiume.

Muhtasari

•Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 26 alisema ni hamu ya mke wake Wema Sepetu kupata mtoto wa kiume.

•Whozu pia alituma ombi kwa mashabiki wao kuwaweka kwenye maombi ili wabarikiwe na mtoto wa kwanza pamoja.

Image: INSTAGRAM// WHOZU

Mwimbaji Oscar John Lelo almaarufu Whozu amefunguka kuwa ni ndoto na maombi yake kupata mtoto na mke wake Wema Sepetu mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki jana, mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 26 alisema ni hamu ya mke wake Wema Sepetu kupata mtoto wa kiume.

Whozu alisema amekuwa akimwomba Mwenyezi Mungu atimize haja ya mioyo yao.

“Ndoto yangu mwakani, mwenyezi Mungu anisaidie mimi na mpenzi wangu Chimama atujalie mtoto, anatamani sana apate mtoto wa kiume na nikamwambia mwenyezi Mungu huyu, hakuna sala ndogo kwa mwenyezi Mungu. Tunaomba sana tupate mtoto, mtoto wetu awe mtoto wa kiume, awe kakae Lola,” Whozu alisema.

Aliongeza, “Ni sala ninalomuomba mwenyezi Mungu. Ni ndoto yangu ya mwakani.”

Whozu pia alituma ombi kwa mashabiki wao kuwaweka kwenye maombi ili wabarikiwe na mtoto wa kwanza pamoja.

Mke wake, Wema Sepetu ambaye alikuwa amesimama kando yake wakati wa mahojiano hayo alisema atakuwa sawa kupata mtoto wa jinsia yoyote.

“Ata akitokea wa kike ni sawa. Akija wa kiume wa kike ni sawa,” alisema.

Wema alisema ni hamu yake kubwa kuvunja utasa wake na kupata mtoto wa kwanza na mpenzi huyo wa maisha yake, Whozu.

"Nimekuwa nikitamani sana mtoto. Lakini chochote kitakachotokea kwanza, iwe mtoto kwanza ama harusi ni sawa," alisema.

Muigizaji huyo mkongwe wa filamu bongo aidha alizungumzia tatizo lake la uzazi ambalo limemzuia kuwa mama hadi sasa.

"Niko na shida ya kizazi. Huwanga nikipata mimba mara nyingi sifiki miezi miwili mitatu mimba inaharibika. Ilitokea, bahati mbaya," alisema.

Huku akizungumzia video iliyosambaa hivi karibuni iliyomuonyesha akiwa mjamzito, Wema alisema kuwa video hiyo ni feki na kufafanua kuwa yeye si mjamzito.

Alisema kuwa video hiyo iliyohaririwa ilimtia hisia sana hivi kwamba hata alitokwa na machozi baada ya kuiona

“Ilinifanya nipate hisia sana. Nilimtumia Chibaba (video) nikamwambia hichi kitu kimenifanya mpaka nikalia. Akaniambia nisijali, ni sawa, ni kitu ambacho ni watu wanakutakia na wanakuombea. Kama wanakuombea basi ni kitu kiko positive. Tukichukulie kama positive,” Wema Sepetu alisema.

Mpenzi  huyo wa zamani wa bosi wa WCB Diamond Platnumz alifichua kuwa kufuatia video hiyo alipokea maswali mengi na jumbe za pongezi kutoka kwa watu walioamini kuwa ni mjamzito baada ya kuiona video hiyo.

Alisema jumbe nyingi alizopokea zilimsukuma kufafanua mambo na kutupilia mbali uvumi huo wa ujauzito.

“Kwangu mimi watu walikuwa wananiuliza sana maswali. Kwa sababu sio watu wengi wanakuwa wananiona mara kwa mara, wengine wakiona video wanaona kweli mimi ni mjamzito. Maswali yalikuwa ni mengi, hongera pia zilikuwa nyingi,” alisema.

Aliongeza, “Ilibidi nipost kitu ili kuwaambia mashabiki wangu na watu ambao wanapenda kwamba sio kile ambacho walikuwa wakifikiria. Lakini kwa kweli nitatamani sana siku moja.”