Wanandoa Bahati na Diana Marua wameachia wimbo wao wa kwanza pamoja.
Bahati na mkewe ambaye katika usanii anajitambulisha kama Diana B wameshirikirana kwenye kibao 'Sweet Love' ambacho kilipakiwa YouTube alasiri ya Jumatatu.
Wimbo huo wa wanandoa hao unazungumzia safari ya mahusiano yao. Wawili yao wanahakikishiana kuhusu upendo wa kila mmoja wao kwa mwenzake.
Kwenye wimbo huo Bahati anakiri kuwa mateka katika jela ya mahaba ya mama huyo wa watoto wake wawili.
"Niite mfungwa wa penzi lako. Mimi mateka mamaa. Niitee mfungwa. Basi nifunge na pingu zako, wewe ndio jela mamaa, niite mfungwa," Bahati anamwambia mkewe kwenye wimbo huo.
Diana kwa upande wake anamshukuru mumewe kwa kumfanya kuwa mama, kumzindua kama mwanamuziki na kutoyasikiliza maneno ya mahasidi wa penzi lao.
Katika kipande chake Diana B pia anasikika akimtupia vijembe Diamond kwa kukubali shinikizo la watu wanaopinga uhusiano wake na Zari.
"Walikwambia mimi ni mzee unichoree. Lakini hukumeza presha kama Chibudee. Ukawacha waongee, wajionee. Ukapandisha mapenzi kama longi ya Mkongo. Hii mapenzi ni hodari, imenijenga utadhani matofari, Sweet love Zuchu huiita sukari, Kitu fresh usiku fogothari," Diana anasema kwenye wimbo huo.
Kibao hicho kimeweza kupata mapokezi mazuri hukukikijizolea takriban views 28,000 ndani ya saa moja baada ya kupakiwa.