Wasanii wa Bongo Juma Jux na Ommy Dimpoz wahusika katika ajali mbaya ya barabarani

Ajali hiyo ilitokea mnamo siku ya kuzaliwa ya mwanamuziki huyo wa Bongo R'n'B.

Muhtasari

•Juma Jux na Ommy Dimpoz walinusurika kifo baada ya gari walimokuwa kuhusika katika ajali mbaya ya barabarani.

•Jux alionyesha video za gari nyeupe aina ya Range Rover iliyohusika katika ajali hiyo na ilionekana kuharibika vibaya hasa kwenye upande.

Juma Jux na Ommy Dimpoz walihusika katika ajali ya barabarani.
Image: INSTAGRAM// JUMA JUX

Siku ya Ijumaa, mastaa wa bongo fleva Juma Jux na Ommy Dimpoz walinusurika kifo baada ya gari walimokuwa kuhusika katika ajali mbaya ya barabarani.

Katika taarifa yake kwenye mtandao wa Instagram, mwimbaji huyo wa kibao‘Enjoy’ alifichua kuwa gari lake lilipata ajali wakati akitokea Kizimkazi kuelekea Nungwi Rocks Visiwani Zanzibar. Ajali hiyo ilitokea mnamo siku ya kuadhimisha kuzaliwa kwa mwimbaji huyo.

Hata hivyo, alisema kwa bahati nzuri kila mtu aliyekuwa kwenye gari hilo yuko sawa isipokuwa mtoto mmoja ambaye alikimbizwa katika hospitali mara moja.

"LEO NI SIKU YANGU YA KUZALIWA NA NIMESURIKA AJALI MBAYA SANA NIKIWA NA OMMY DIMPOZ TUKITOKEA KIZIMKAZI - ZANZIBAR KWA MAMA TUKIELEKEA NUNGWI - KENDWA ROCKS KWAAJILI YA SHOW YETU YA JUMAMOSI FULLMOON ALL WHITE PARTY!,” Juma Jux alisema katika taarifa.  

Aliongeza, “NASHUKURU MWENYEZI MUNGU WATU WANGU NA TEAM YANGU YOTE IPO SALAMA, NI MTU MMOJA TU MTOTO AMEKIMBIZWA HOSPITAL LAKINI KWA UWEZO WA MWENYEZI MUNGU NAAMINI ATAKUWA SALAMA!🙏🏾🙏🏾🙏🏾!”

Kuthibitisha hayo, alionyesha video za gari nyeupe aina ya Range Rover iliyohusika katika ajali hiyo na ilionekana kuharibika vibaya hasa kwenye upande.

Mwanamuziki huyo alifichua habari hizo alipokuwa akimuomboleza mwimbaji wa Tanzania Haitham Kim aliyefariki Ijumaa mchana.

Kim ambaye katika siku za hivi majuzi amekuwa akipokea matibabu maalum baada ya kupata matatizo ya kupumua aliaga dunia katika hospitali ya Rufaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, mwendo wa saa sita mchana siku ya Ijumaa.

Marehemu alimuacha nyuma mpenzi wake na mtoto mmoja.

Kifo chake kilitokea siku chache tu baada ya wasanii wa Bongo kuanzisha kampeni ya kuchangisha pesa kwa ajili ya matibabu yake ya gharama.

Iliripotiwa kuwa marehemu alikuwa amekumbwa na matatizo ya kupumua ambapo ilianza kama homa ya kawaida lakini baadaye akawa anakosa pumzi hadi kulazwa.

Mashabiki, marafiki, wanafamilia na watu wengine wa karibu wameendelea kumuomboleza mwimbaji na mwandishi huyo wa nyimbo.Wasanii wengi wa Bongo wakiwemo Nandy, Zuchu, Kajala Masanja, Hamisa Mobetto,Wema Sepetu ni miongoni mwa wasanii wengine wengi pia wamemuomboleza mama huyo wa mtoto mmoja.