"Wewe ni kila kitu kwangu” Guardian Angel amsherehekea Esther Musila kimahaba akitimiza 53

Bi Musila alibainisha kwamba Guardian Angel alibadilisha maisha yake kuwa bora walipokutana.

Muhtasari

•Guardian Angel alitaja miaka mitatu ambayo wamekuwa pamoja kuwa sehemu bora zaidi ya maisha yake.

•Esther Musila alimshukuru mwaimbaji huyo mwenye umri wa miaka 34 kwa kuja katika maisha yake. 

Image: INSTAGRAM// ESTHER MUSILA

 Leo hii, Mei 25, mkewe mwanamuziki Guardian Angel, Bi Esther Musila anaadhimisha siku yake ya kuzaliwa ya 53.

Huku akimsherehekea mkewe kwa kupiga hatua nyingine maishani, Guardian Angel ambaye kwa jina halisi ni Peter Omwaka alitaja miaka 3 ambayo wamekuwa pamoja kuwa sehemu bora zaidi ya maisha yake.

Mwimbaji huyo alisherehekea upendo wao na kumtakia mama huyo wa watoto wakubwa kheri ya siku ya kuzaliwa.

"Siwezi kuamini kuwa imekuwa miaka 3 tayari. Imekuwa sehemu bora zaidi ya maisha yangu. Kukupenda ni hisia tamu zaidi kuwahi kutokea. Unachangamsha dunia yangu malkia wangu. Baraka kwenye siku yako ya kuzaliwa @esther.musila. Wewe ni kila kitu kwangu," Guardian Angel alimwambia mkewe kupitia Instagram.

Guardian Angel aliambatanisha ujumbe wake na bango nzuri la kusherehekea siku ya kuzaliwa ya malkia huyo wake.

Katika jibu lake, Esther Musila alimshukuru mwaimbaji huyo mwenye umri wa miaka 34 kwa kuja katika maisha yake. Alibainisha kwamba Guardian Angel alibadilisha maisha yake kuwa bora walipokutana.

"Maisha yangu yalianza nilipokutana na wewe mpenzi wangu, imekuwa miaka 3 ya furaha na nakushukuru kwa kuja. Umeleta maana mpya kabisa ya uwepo wangu. Nakupenda mfalme wangu," Bi Musila alijibu.

Huku akijisherehekea kwenye ukurasa wake, Bi Esther Musila ambaye ni mzaliwa wa kwanza wa wazazi wake alifichua kwamba alitokea katika familia ya chini, hali ambayo ilichangia yeye kuwa mtu aliye leo.

"Nimepitia mengi maishani, nimeyaona na kuyasikia!! Kitu kimoja ninachoshukuru ni kuwa, siku zote nimesimama kivyangu na kufuata sheria zangu, najua kinachomfaa Esther na ndicho ninachompatia, bora zaidi kwake. Sijawahi kukwepa kuishi maisha yangu na kuyaishi bila msamaha! Ninastawi kwa uchanya na hisia nzuri kwa kuwa nina makusudi katika ninacholisha akili, mwili na roho yangu." alisema.

Mhasibu huyo aliweka wazi kwamba anajivunia umri wake kwa kuwa anafahamu fika kwamba ni Mungu aliyemfikisha pale.

Aidha, aliwashukuru wote ambao wameendelea kusimama naye na kumuonyesha upendo wakiwemo wanafamilia na marafiki.

"Kwa Esther, endelea kushinda, kuishi, kupenda na kucheka. Wewe ni Bora tu! Heri ya siku ya kuzaliwa kwangu," aliandika.