Willis Raburu na mkewe Ivy Namu wamtambulisha binti yao mchanga kwa mara ya kwanza (+picha)

Wameonyesha sura ya binti yao Yara na kukiri wameridhishwa na maendeleo yake.

Muhtasari

•Yara ambaye alikuwa amelazwa kwenye mkeka mdogo alikuwa amevalishwa nguo nyekundu na ameshika mdoli mikononi mwake.

•Wazazi hao wa watoto wawili walieleza kuridhishwa kwao na maendeleo ya binti huyo wao mdogo.

Wachumba Willis Raburu na Ivy Namu kwa mara ya kwanza wameonyesha sura ya binti yao wa miezi mitatu kwa umma.

Wawili hao walichapisha picha nzuri ya binti huyo mrembo kwenye kurasa zao za Instagram siku ya Jumamosi asubuhi.

"Salamu za msimu kutoka kwa Raburu mdogo, mtoto wetu mzuri Yara 😘," waliandika chini ya picha hiyo.

Pichani, mtoto huyo ambaye alikuwa amelazwa kwenye mkeka mdogo alikuwa amevalishwa nguo nyekundu na ameshika mdoli mikononi mwake. Tabasamu zuri liliweza kuonekana kwenye uso wake.

Aidha, Wazazi hao wa watoto wawili walieleza kuridhishwa kwao na maendeleo ya binti huyo wao mdogo.

"Neema zote za Mungu katika uso mmoja mdogo .. alikuwa na umri wa wiki 7 hapa (pichani) , sasa ana umri wa miezi mitatu, ni mzuri na mnene kama siku zote, mioyo yetu imejaa," Namu na Raburu walisema.

Haya yanajiri siku moja tu baada Bi Nam kufunguka kuwa kwa wiki kadhaa tangu kumpokea mtoto wa pili, amekuwa akilemewa sana kusawazisha katia ya mambo tofauti kwenye maisha yake – haswa kutokana na jukumu gumu la kumlea mtoto mchanga.

Namu kupitia Instastory yake, aliandika ujumbe mrefu akieleza jinsi ulezi umemtwika jabali zito kichwani huku akishindwa hata kujizingatia mwenyewe na hata kutangamana na marafiki zake kwenye mitandao ya kijamii, kinyume na ilivyokuwa awali akiwa bado hajapata mtoto.

“Kwa wiki kadhaa zilizopita nimekuwa nikijihisi kulemewa kabisa kutokana na kuwa karibu na kwa makusudi yote na wanangu, na pia kupata muda wangu binafsi pia. Na pia kupakia vitu hapa ndio kumepata pigo kubwa zaidi, na kwa kweli sijielewi kabisa na hilo,” Namu alisema.

Alizidi kuelezea kwamba sasa imembidi kufuata mkondo huo wa kutokuwa sana mitandaoni kutokana na jukumu kubwa la kuwaangalia watoto wake wawili ambao wameachana kwa miezi kadhaa tu.

“Kwa hiyo ninaenda tu na mkondo huo wa kupakia mara chache, ninachokitaka sasa hivi ni kupata nafasi ya kupumua basi tosha. Lakini watoto wawili si wachache, kusema kweli ni kazi ngumu sana kuwalea watoto. Pongezi kwa wazazi wote mnaoendeleza uzazi kwa kuwa karibu na watoto wenu, mnafanya kazi kuntu.”

Miezi kadhaa iliyopita, Namu na Raburu walitangaza kupata mtoto wa pili wa kike takribani mwaka mmoja na miezi ya kuhesabika tangu kumkaribisha mtoto wa kwanza wa kiume waliyempa jina Mali.