Yesu wa Tongaren avunja kimya baada ya Wakenya kusikia kilio chake cha msaada

Mchungaji huyo aliwasisimua wanahabari baada ya kuwaomba wamsaidie kununua jiko la gesi na simu.

Muhtasari

•Bw Simiyu alikiri kwamba anatatizika kifedha na hivyo kuwaomba watu wema kumsaidia kugharamia elimu ya watoto wake.

•Bw Simiyu aliachiliwa huru siku ya Jumanne asubuhi baada ya mahakama ya Bungoma kubaini hana kesi ya kujibu.

akizungumza na wanahabari mnamo Mei 16, 2023.
Yesu wa Tongaren akizungumza na wanahabari mnamo Mei 16, 2023.
Image: HISANI

Mchungaji wa Bungoma mwenye utata mwingi Eliud Simiyu almaarufu Yesu wa Tongaren ametoa shukrani za dhati kwa Wakenya wenye mapenzi mema ambao wameendelea kumchangia kwa kusikia ombi lake la msaada.

Siku ya Jumanne, baada ya kuachiliwa huru na mahakama ya Bungoma, Bw Simiyu alikiri kwamba anatatizika kifedha na hivyo kuwaomba watu wema kumsaidia kugharamia elimu ya watoto wake.

Mchungaji huyo pia aliwasisimua waandishi wa habari baada ya kuwaomba wamsaidie kununua jiko la gesi  na simu.

"Alafu nawaomba Wakenya, msione Yesu wa Tongaren anatrend sana mkafikiria ako na mali. Mimi si YouTube Content Creator, mimi nimemaanisha kwa ajili ya kazi ya Mungu. Asante," Bw Simiyu aliwaambia wanahabari.

Ni wazi kuwa Wakenya walisikia kilio cha mchungaji huyo kwani baadaye alithibitisha kwamba alikuwa ameanza kupokea michango.

Katika kipindi cha moja kwa moja kwenye Tiktok, Bw Simiyu aliwashukuru wale ambao wametuma msaada na kutangaza baraka kwao.

"Namba ya simu ni 0794 749 216. Iwapo umetuma, shukran kwa msaada wako, italeta jina Totsi Simiyu. Hiyo ni namba ya Yesu wa Tongaren.

Nashukuru kwa msaada wenu kwa ajili ya watoto wangu shuleni. Hata wale wanaendelea kunitumia 50, 100, 1000. Nimefurahia Mungu awabariki," Yesu wa Tongaren alisema kwenye Tiktok siku ya Jumanne.

Bw Simiyu aliachiliwa huru siku ya Jumanne asubuhi baada ya mahakama ya Bungoma kubaini hana kesi ya kujibu.

Hii ni baada ya serikali kusema hakuna ushahidi wa kutosha wa kumshtaki.

Alikuwa ameshutumiwa kwa uendeshaji kinyume cha sheria wa jamii isiyosajiliwa, misimamo mikali na ulaghai wa fedha lakini Jumanne upande wa mashtaka ulisema hauna ushahidi.

Kiongozi wa Chama cha Roots, George Wajackoyah alimwakilisha Yesu wa Tongaren mahakamani.

Simiyu alikuwa amezuiliwa na polisi kwa siku nne zilizopita ambapo alifanyiwa uchunguzi wa kiakili, baada ya kutangazwa kuwa na matatizo ya kiakili.

"Mahakama imekubali na kutoa kibali kwa upande wa mashtaka kumzuilia mshukiwa kwa siku nne zaidi ili kuwaruhusu kukamilisha uchunguzi na kufanya tathmini ya kiakili," Olando alisema.