Binti ya mfanyibiashara Mike Sonko, Sandra Mbuvi almaarufu Thicky Sandra ametoa ombi kwa Wakenya kutomshambulia baba yake kufuatia video yake akionyesha mamilioni ya pesa ndani ya nyumba yake ambayo imesambazwa mitandaoni.
Wakenya kwenye mitandao ya kijamii wamekuwa wakitoa hisia mseto baada ya gavana huyo wa zamani wa kaunti ya Nairobi kuonekana katika video akijigamba kuhusu noti za pesa za Kenya na dola za Marekani alizofadhi nyumbani kwake.
Katika video hiyo, Sonko alionekana akifungua masanduku makubwa yaliyojaa pesa huku akimsuta mtu asiyetambulishwa kwa kutilia shaka utajiri wake.
"Ati sina pesa kwa sababu sisaidi watoto... Nani ali kwambia sina pesa!?" Sonko kwa hasira tele alimfokea mtu huyo ambaye hakutajwa jina ambaye bila shaka alikuwa amemkera sana hadi kwenye koo.
"Sina pesa ya kusaidia watoto. Hii pesa ni ya kuharibu mabibi wangu!" mwanasiasa huyo asiyepungukiwa na drama alisema huku akionyesha mamilioni ya pesa ambazo alisema ni za kujaza mafuta kwenye magari yake.
Kwa maneno yake mwenyewe, gavana huyo wa zamani alidai kuwa alikuwa akihifadhi zaidi ya milioni 30 kwenye nyumba.
Tangu video hiyo kuchapishwa mitandaoni, Wakenya wamekuwa wakitoa maoni mseto, baadhi wakimshambulia huku wengine wakimtetea.
Bi Sandra ambaye bila shaka hakufurahishwa na mashambulizi dhidi ya baba yake amewaomba Wakenya kumuelewa huku akibainisha kwamba ni kawaida kwa mtu yeyote kupandwa na hasira katika nyakati fulani.
"Jamani naomba muache kumshambulia baba yangu kwenye hiyo video. Kila mtu anakasirika na kama ungekuwa wewe kwenye nafasi hiyo ungepinduka zaidi," Sandra alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.
Aliongeza, "Nyinyi nyote hamuoni mambo kwa mtazamo wake lakini mna haraka sana kufikia hitimisho. Yeye ni binadamu naomba!"
Video ya Sonko imezua hisia mseto kutoka kwa Wakenya huku kundi lao likiibua maswali kuhusu kazi ambacho gavana huyo wa zamani anafanya ili kumudu maisha ya kifahari ambayo anaishi.