Zuchu alazimika kusitisha shoo baada ya kurushiwa jiwe usoni akiwa kwenye steji

Zuchu alikuwa ametoka kuwasalimia mashabiki na alikuwa akijiandaa kutumbuiza ndipo jiwe lilipomtua usoni.

Muhtasari

•Zuchu mnamo siku ya  Ijumaa jioni alilazimika kusitisha shoo yake kwa muda baada ya kupigwa na jiwe usoni.

•Walinzi waliokuwa wamesimama karibu walionekana wakimuelekeza kutoka jukwaani hadi mahali pa usalama huku kelele zikiongezeka kutoka kwa umati.

Image: INSTAGRAM// WASAFI MEDIA

Malkia wa Bongo Zuhura Othman almaarufu Zuchu mnamo siku ya  Ijumaa jioni alilazimika kusitisha shoo yake kwa muda baada ya kupigwa na jiwe usoni.

Msanii huyo wa WCB alipanda jukwaani kutumbuiza na alipokuwa akiwasalimia mashabiki waliojitokeza kwenye tamasha la VIP-Pre-Party lililofanyika mjini Mbeya, Tanzania, jiwe lililorushwa kutoka kwenye umati  lilitua usoni mwake

“Mbeya mambo..” Zuchu alisikika akiwaambia mashabiki kabla ya kusimama mara moja na kuinamisha uso wake chini baada ya kugongwa.

Walinzi waliokuwa wamesimama karibu walionekana wakimuelekeza kutoka jukwaani hadi mahali pa usalama huku kelele zikiongezeka kutoka kwa umati.

Baada ya kufanyiwa tathmini na kuthibitishwa kuwa hakujeruhiwa vibaya na jiwe hilo, mwimbaji huyo mzaliwa wa Zanzibar alirejea jukwaani na kuendelea kuwapa raha mashabiki wake kwa vionjo vya nyimbo zake nzuri ukiwemo wa hivi majuzi wa ‘Honey.

WCB walikuwa wameandaa shoo iliyopewa jina la ‘’V.I.P PRE-PARTY'  katika City Pub Mbeya kabla ya tamasha la Wasafi Festival lililopangwa kufanyika siku ya Jumamosi jioni. Karamu hiyo ilipambwa na wasanii waliopangwa kutumbuiza kwenye tamasha la Wasafi Festival, toleo la Mbeya .

Wasanii wengine waliotumbuiza kwenye pre-party hiyo ya Ijumaa jioni ni pamoja na bosi wa WCB, Diamond Platnumz, Lavalava na Mbosso ambao wote wapo chini ya Wasafi Records. Wanne hao walipiga shoo la kusisimua na mashabiki walisikika wakiwashangilia walipokuwa wakipanda jukwaani mmoja baada ya mwingine.