Mahakama,Tanzania yakubali kusikiza hoja ya Lissu kupinga kuvuliwa ubunge

Mahakama Kuu nchini Tanzania imekubali kusikiliza hoja za mwanasiasa mwandamizi wa upinzani Tundu Lissu kupinga kuvuliwa ubunge.

Lissu, kupitia kaka yake Alute Mughwai amefungua shauri Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam akipinga uamuzi wa Spika Job Ndugai kumfuta ubunge.  Hata hivyo, mawakili wa serikali iliweka pingamizi wakitoa hoja nane wakitaka ombi la Lissu kutupiliwa mbali na mahakama.

Shauri hilo lipo mbele ya Jaji Sirilius Matupa, ambaye hii leo ameamua kuendelea kusikiliza hoja za Lissu.

Lissu alifutwa ubunge wa jimbo la Singida Mashariki Juni 28, 2019 baada ya Spika Job Ndugai kutoa maelezo kuwa hajulikani alipo na hakusaini fomu za maadili.

Gazeti la Mwananchi linaripoti kuwa katika kesi hiyo serikali ya Tanzania ina mawakili mawakili 15 dhidi ya wanne wa Lissu. Huu ni mwanzo wa wa hoja na vita ya kisheria mahakamani ambapo upande wa Lissu utapigana kuthibitisha uhalali wake wa kuendelea kusalia na ubunge huku upande wa mawakili wa serikali kuonesha kuwa Spika Ndugai alikuwa sahihi katika maamuzi yake.

Awali, BBC ilizungumza na Lissu ambaye amedai kuwa amefutwa ubunge huku ikifahamika wazi kuwa amekuwa nje kwa matibabu tangu tarehe 7 mwezi Septemba mwaka 2017, baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana.

Lissu amesema kwa mujibu wa sheria na taratibu za bunge la Jamuhuri ya muungano wa Tanzania, wajibu wa kutoa taarifa kuhusu mbunge anayeumwa sio wajibu wa mbunge mwenyewe, ni wajibu wa waganga walioajiriwa na bunge.

''Kwa hiyo Bunge lilikuwa na wajibu wa kujua muda wote tangu tarehe7 mwezi Septemba mwaka 2017 kuhusu maendeleo yangu afya''.

''Walitakiwa kuja Nairobi sikuwaona, walisema wangekuja hawakuja, walitakiwa waje Ulaya hawakuja, hivyo waliovunja sheria si mimi ni wao''.

Lissu amesema alitarajia hatua zilizochukuliwa na spika kutokea kwa sababu alishasema kwa hiyo ilipotokea mwezi wa sita wala haikua ajabu.

''Mtu ambaye alishakuwa na nia ya kunifuta ubunge nisingeweza kumzuia, vinginevyo labda ningesema niachane na habari ya matibabu nirudi Tanzania''.