Pasta Ng'ang'a mashakani kwa kutishia kudhoofisha nyeti za wanaume kanisani

Mhubiri anayezingirwa na utata kila kuchao Pasta Ng’ang’a ameshtakiwa kwa kuwatishia na kutumia lugha ya matusi dhidi ya wanaume katika kanisa lake.

Kulingana na kesi iliyowasilishwa, mhubiri huyo wa televisheni anashtumiwa kwa kutumia lugha isiofaa akiwalenga waumini wa kiume katika kanisa lake kwa misingi ya sadaka wanayotoa kanisani.

Lugha hiyo huenda ikavuruga amani katika kanisa hilo, hasa baada ya kuwaita waumini hao “ng’ombe wewe” na “ng’ombe hizi” usemi ambao huelekezwa mtu mpumbavu.

Matamashi ya Ng’ang’a yamesekana kuwa ya kudunisha na kudhalilisha kuhusiana na nyeti ya wanaume na kuzilinganisha na kidole cha mwisho kwenye kiganja“kakitu” na “tuvitu”.

"Katika tarehe unayoifahamu na bila sababu ulizua hali ya swintofahamu na kutishia kuvuruga utulivu kanisani na hasa kwa kutishia kulemaza nguvu za kiume za wateja wetu ili wasiweze kujamiana na wake wao kwa kutumia mbinu ambazo hukutaja,” Barua ya mawakili wa kampuni ya uakili ya Otieno and Amisi ilisema.

Amisi ni wakili anayewakilisha wanaume katika kanisa la Neno Evangelism Ministries. Barua hiyo ilisema kwamba matendo ya Ng’ang’a yalishusha hadhi ya wateja wake katika jamii na kuwafanya waonekane wadhaifu na waoga, wasiokuwa na fikra na wenye vijidude vya kiume vidogo kuliko wanaume wenzao.

Mhubiri huyo ametakiwa kuondoa vitisho vyake kupunguza nguvu za kiume za wanaume katika kanisa lake.