Uchumi wa rasilimali za baharini ni muhimu kwa maendeleo ya Kenya - Uhuru

Rais Uhuru Kenyatta amesema Kenya inaendelea kutoa kipaumbele kwa utekelezaji wa mipango ya uchumi wa rasilimali za baharini kutokana na uwezo wa sekta hiyo wa kuleta maendeleo ya haraka nchini.

Rais alisema rasilimali za nchi kavu zinazopungua  hazitatosha kikamilifu kudumisha idadi ya watu ulimwenguni inayoendelea kuongezeka kwa kipindi kirefu kijacho na hivyo kuna haja kwa mataifa kuzingatia uchumi wa rasilimali za baharini katika mipango ya maendeleo.

"Mwanzo kabisa, wengi wetu tulitambua bayana rasilimali ambazo zitakuwepo hususan wakati huu wa mabadiliko ya hali ya anga kutokana na rasilimali za nchi kavu ambazo tumeemdelea kumaliza kwa mwendo wa pole pole kupitia idadi kubwa ya watu na kuenea kwa jangwa kati ya maswala mengine mengi," kasema Rais.

Rais ambaye alizungumza wakati wa mkutano wa Mataifa Yanayostawi ya Visiwa Vidogo uliofanyika pembezoni mwa Kikao cha 74 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Jijini New York, alisema Kenya iko makini kustawisha uchumi wake wa rasilimali za baharini kutokana na uwezo mkubwa wa sekta hiyo kwa uchumaji wa mali pamoja na kubuni nafasi za ajira.

"Imetimia kwamba siku zetu za baadaye pia zinategemea jinsi tutakavyoweza kubainisha rasilimali za bahari zetu. Kwa kufanya hivyo, tulitambua uwezo mkubwa wa bahari zetu kwa ukuaji wa uchumi, maendeleo na ajira. Na pia rasilimali za vyakula na utajiri mkubwa chini ya ardhi," kasema Rais Kenyatta.

Alisema wajibu wa Kenya wa kupigia debe maendeleo ya kudumu ya ustawi wa uchumi wa baharini ulimwenguni unatokana na kutambua kwamba bahari ni muhimu kwa siku za baadaye za binadamu.

"Bahari zetu ni sehemu muhimu kwa siku za baadaye za binadamu na ndio maana tulimalizia kwa kusema kwamba huku tunapolenga siku zijazo hili sharti liwe swala la kipaumbele kwa kila raia ulimwenguni. Tusipofanya hivi hatutapoteza tu rasilimali, lakini muhimu zaidi tutapoteza maisha na vizazi vijavyo," kasema Kiongozi wa Taifa.

Akizungumza kuhusu kongamano la uchumi wa kudumu wa rasilimali za baharini ambalo liliandaliwa na Kenya kwa ushirikiano na Canada pamoja na Japan Jijini Nairobi mwaka uliopita, Rais Kenyatta alisema uchumi wa kudumu wa rasilimali za baharini unawezekana kwa kushirikisha washika dau wote.

"Kitu cha kwanza kilichomjia kila mmoja lilikuwa swala la udumishaji na kutambua kwamba inatupasa sote kuwajibika kwa pamoja ili kutimiza malengo tunayoazimia," kasema Rais.

Rais alisema kwamba mkutano wa Nairobi uliohudhuriwa na wajumbe 1,600 ulifaulu kuwaleta pamoja washika dau wa uchumi wa rasilimali za baharini kuanzisha mchakato wa ushirikiano na kufanya kazi kwa pamoja kutimiza maendeleo ya kudumu na kutumia sekta hiyo kwa ustawi wa kiuchumi.

"Swala moja muhimu lililofanyika Jijini Nairobi lilikuwa uwezo wa kuwaleta pamoja washikadau mbalimbali kuhusiana na uchumi wa rasilimali za baharini. Tulikuwa na wanasayansi wetu. Tulikuwa na wajasiriamali wetu. Serikai ziliwakilishwa. Mashirika ya kijamii yaliwakilishwa. Makundi ya wachache yaliwakilishwa," kasema Rais Kenyatta.

Akizungumza kuhusu uwezo wa ushirikiano katika kufanikisha maendeleo ya kudumu ya sekta hiyo, Rais alitoa mfano wa mpango unaoungwa mkono na Serikali hapa nchini ambapo makundi ya wanawake yanajipatia riziki kutokana na malipo ya gesi ya kaboni inayotokana na uhifadhi wa mikoko.

Alisema licha ya changamoto zinazokabili uchumi wa rasilimali za baharini kama vile mabadiliko ya hali ya anga, sekta hiyo ina uwezo wa kunufaisha chumi kote ulimwenguni na akatoa wito wa kushirikisha zaidi sekta ya kibinafsi.

"Licha ya kukabiliwa na changamoto, ni bayana kuna nafasi kubwa za kunufaisha kila mmoja wetu. Huu ni wakati ambapo tunapaswa kuanza kulenga maswala ya mabadiliko ya hali ya anga, ya hatari zinazotukabili na tuanze kuzingatia nafasi zilizopo.”

"Tunapotambua pakubwa juhudi za kujitolea, kuna nafasi kubwa kwa sekta ya kibinafsi kuchangia zaidi ajenda hiyo tuliyo nayo na kutimiza maendeleoe," kasema Rais.