Uhuru akutana na viongozi wa Mt Kenya, orodha ya watakaozungumza

MT.KENYA.LEADERS
MT.KENYA.LEADERS
Rais Uhuru Kenyatta anaongoza mkutano unaoleta pamoja na viongozi wa eneo la Mlima Kenya hivi leo katika jitihada zake kutuliza uasi katika ngome yake.

Uhuru anatarajiwa kupigia debe mwafaka wake na kinara wa upinzani Raila Odinga ambao umekuwa ukipingwa na viongozi wanaoegemea mrengo wa naibu rais William Ruto.

Mkutano huo unafanyiwa ikulu ndogo ya Sagana katika kaunti ya Nyeri na walioalikwa wanajumuisha magavana, maseneta, wabunge,wakilishi wadi, makamishna wa kaunti na wawakilishi wa sekta mbali mbali.

Viongozi kadhaa wameratibiwa kuhutubia mkutano huo. Kulingana na ratba rasmi, aliyekuwa seneta wa Nyeri Mutahi Kagwe atakuwa msimamizi wa itifaki. Mkutano huo utaanza baada ya maombi kutoka kwa mhubiri Peter Munga ambaye pia anawakilisha baraza la wazee wa Agikuyu.

Wambui Nyutu atazungumza kwa niaba ya vijana kutoka eneo hilo akieleza changamoto wanazokumbana nazo kama vijana wa eneo hilo. Aliyekuwa mwenyekiti wa Benki ya Equity Peter Munga pia atakuwa mmoja wa watu watakao toa hotuba muhimu, akiwakilisha sekta ya kibiashara.

Polycarp Igathe, ambaye ni naibu rais wa Vivo Energy barani Afrika atawakilisha wataalam wa nyanja mbali mbali kutoka eneo hilo.

Mbunge wa Nyeri Town Ngunjiri Wambugu atazungumza kwa niaba ya wabunge wa Mt Kenya.

Wambugu ni mbunge wa Jubilee anayeegemea upande wa mrengo wa kieleweke ambao unaunga mkono mchakato wa BBI na ushirikiano baina ya rais Kenyatta na Raila.

Seneta wa Embu Njeru Ndwiga atazungumza kwa niaba ya maseneta katika mkutano huu, Gavana wa Nyeri Mutahi kahiga na mwenzake Anne Waiguru wa Kirinyaga watazungumza kwa niaba ya magavana.

Pia patakuwepo muakilishi kuzungumza kwa niaba ya maendeleo ya wanawake na muungano wa wenye matatu kutoka eneo hilo.

Mkutano huo pia utahutubiwa na mawaziri Joe Mucheru (ICT), James Macharia (Uchukuzi), Sicily Kariuki (Afya), Margaret Kobia (Utumishi wa umma) na makatibu wa kudumu Karanja Kibichu na Kirimi Kaberia.

Ganava wa Meru Kiraitu Murungi pia atahutubia mkutano huo kabla ya kumualika rais kutoa hotuba yake.