Washauri wa Mudavadi wanamchimbia kaburi la kisiasa-Wazee wasema

mudavadi 1
mudavadi 1
Washauri wa Musalia Mudavadi wanamchimbia kaburi la kisiasa  kwa kumpa ushauri ambao haumsaidii wamesema wazee  kutoka eneo bunge la Luanda .

Wamesema Mudavadi hatofaulu katika azma yake ya kuwa rais endapo hatokoma kuwashambulia viongozi  wa ngazi ya chini katika chama cha ANC walio na uwezo wa kumsaidia kuafikia ndoto yake yake ya kuwa rais .

Wakiongozwa na  Livistone Omwakwe,  wazee hao waliokuwa wakizungumza katika  Central Villa Hotel  Mjini Luanda siku ya ijumaa  wamesema  Mudavadi anahitaji msaada wa viongozi wote kutoka eneo hilo ili kuweza kuiga jeki jitihada zake za kuongoza nchi .

Hii ni baada ya  habari kwamba chama cha ANC kimemfurusha  seneta wa kakamega Cleopahs Malala kwa kukaidi msimamo wa chama wakati wa uchaguzi mdogo wa kibra mwaka jana ambapo alimuunga mkono mgombeaji wa  ODM  Imran Okoth  badala ya mgombeaji wa ANC  Eliud Owalo .

ANC  pia kimefurusha mbunge mteule  Geoffrey Osotsi. Chama hicho kimedai kwamba alitumia vibaya pesa za chama na kukiuka kanuni za ANC .

Lakini wazee hao  wamepuuza madai hayo dhidi ya  Osotsi,  wakisema hangeweza kutoa pesa za chama bila idhini ya mwenyekiti au mweka hazina ambao sahihi zao zinahitajika .

Omwakwe  amesema Mudavadi anafaa kufanya kazi na wanachama wote wa ANC   na vongozi wao ili kukiboresha chama hicho kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022 .