3 watekwa nyara na wanamgambo wa Al Shabaab Mandera

Watu watatu hawajulikani waliko baada ya kutekwa nyara na washukiwa kundi la kigaidi la Al Shabaab katika kaunti ya Mandera siku ya Jumatano jioni.

Polisi wanasema kwamba wahasiriwa ni mafundi na walikuwa safarini kuelekea eneo la Lafey kufanya kazi.

Kisa hicho kilitokea umbali wa kilomita 30 kutoka mji wa Lafey wakati gari la usafiri wa umma ambamo watatu hao walikuwa wakisafiria lilisimamishwa na watu waliokuwa wamejihami kwa silaha kali.

Watatu hao ambao si wenyeji walikuwa wageni katika eneo hilo na kwa sasa haijulikani waliko.

Vikosi vya usalama vimeanzisha oparesheni ya kuwasaka huku hali wasi wasi ikitanda kwa hofu kuwa huenda wanamgambo wa Al Shabaab wako katika eneo hilo.

Kuna hofu pia kwamba huenda kisa hicho kimechangiwa na malumbano ya kisiasa katika eneo hilo.