Ushirikiano bora wa kimataifa ni muhimu katika kukabili changamoto za kimataifa

Uhuru.1 (2)
Uhuru.1 (2)
Rais Uhuru Kenyatta amesema kwamba utangamano muafaka katika mfumo wa kimataifa unaozingatia sheria, ni muhimu katika kukabili changamoto zinazokumba ulimwengu ikiwemo kuleta amani na ufanisi.

Rais Kenyatta siku ya Jumatano alisema ulimwengu unaweza kutatua matatizo magumu yaliyoko wakati huu ikiwemo janga la kiafya la Covid-19 kupitia ushirikiano thabiti wa kimataifa.

“Kenya inaamini kwa dhati kwamba iwapo tutaendelea kujikita katika utangamano wa kimataifa wenye nia moja, na iwapo tutakuwa wa haraka kuzingatia mabadiliko na mageuzi bora, iwapo tutadumu katika mfumo unaozingatia sheria na kufanya mambo kwa ubunifu na bila ubinafsi, tutaweza kushinda changamoto zetu na kujipatia usalama, amani ya kudumu na ufanisi kwa wote," kasema rais Kenyatta.

Kiongozi wa Taifa alitoa mfano wa Malengo ya Maendeleo ya Kudumu ya Umoja wa Mataifa (SDGs) kuwa mtindo wa kitendo cha utangamano wa kimataifa unaodhirisha ari ya ulimwengu ya kukomesha umaskini, kuhifadhi mazingira na kuhakikisha ufanisi kwa watu wote.

“Changamoto zinazotukabili leo zinathibitisha haja ya kujitolea kwetu katika kutekeleza Malengo ya Maendeleo ya Kudumu ya Umoja wa Mataifa hasa katika kupigana na umaskini na ukosefu wa usawa lakini pia jukumu letu la pamoja la kuchangia kikamilifu ndoto hii ya pamoja,” kasema Rais Kenyatta.

Rais alitoa hotuba yake kupitia njia ya video Jumatano jioni wakati wa majadiliano kwa njia ya video kwa kikao kinachoendelea cha 75 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Huku akielezea haja ya ulimwengu kuwa tayari kukabiliana na ongezo la majanga ulimwenguni, Rais Kenyatta alisema ugonjwa wa korona unafaa kuwapa motisha kuimarisha juhudi za pamoja katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.

“Janga la Covid-19 na changamoto za sasa ikiwemo suala la tatizo la tabia nchi na mazingira na viumbe na uhasama unaoongezeka kati ya mataifa yanayoegemea pande mbali mbali, ukosefu wa usawa wa kijamii na kiuchumi, tatizo la uhalisi na utawala na vile vile matatizo yanayotokana na dunia ya kidijitali, bila shaka yamedhihirisha haja ya utangamano wa kimataifa katika kuchukua hatua ya pamoja,” kasema Rais.

Rais alisema Kenya inatekeleza mkakati muafaka wa kukabili janga la korona ambao unajumuisha ufufuzi na upanuzi wa mifumo ya afya katika kaunti na kitaifa.

Alisema Kenya imechukua hatua kuthibiti masuala ya kifedha na ushuru ili kulinda uchumi na biashara nchini kutokana na athari mbaya za janga hilo la kiafya ulimwenguni.

Katika bara hili, Rais Kenyatta alisema Kenya inashirikiana kwa karibu na mataifa mengine wanachama wa Muungano wa Afrika katika kutuoa muongozo wa pamoja wa kukabiliana na virusi vya ugonjwa wa Korona.

“Tulichukua mkakati wa pamoja wa kukabili virusi vya korona ambapo tumefaulu vilivyo katika kushirikisha juhudi za bara nzima za kuzuia maradhi makali na vifo vinavyotokana na ugonjwa huo wa COVID-19 mbali na kutusaidia kupunguza vurugu za kijamii na kiuchumi,” kasema Rais.

Alisema akiwa kiongozi wa kundi linalojumuisha mataifa 97 ya Afrika, Pacific na Caribbean, Rais Kenyatta alisema amefahamu vyema zaidi siasa za ulimwengu na mashindanio yaliopo ambayo hayazingatii hatua za kujenga ulimwengu bora, thabiti, salama, wenye raia walio na afya na ufanisi.

Hivyo basi, Rais alisema ni muhimu hata baada ya kushughulikia janga la korona, ulimwengu wapaswa kudumisha umoja katika ufufuzi wa kiuchumi.