logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Rais Samia Suluhu Hassan: Nukuu zake tano zilizowafurahisha Wakenya

Rais mpya wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amekuwa akitoa matumaini - akijaribu kuimarisha uhusiano na taifa jirani la Kenya ambalo lilipata pigo wakati wa uongozi wa mtangulizi wake .

image
na Brian Ndungu

Habari08 May 2021 - 09:00

Muhtasari


    rais samia suluhu. Picha: BBC

    Rais mpya wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amekuwa akitoa matumaini - akijaribu kuimarisha uhusiano na taifa jirani la Kenya ambalo lilipata pigo wakati wa uongozi wa mtangulizi wake .

    John Magufuli aliyefariki mwezi Machi alikuwa akipinga uwepo wa virusi vya corona na msimamo wake uliilazimu Kenya kufunga mipaka yake .

    Lakini akiwa katika ziara yake ya siku mbili nchini Kenya Bi Samia aliacha utamaduni wa Tanzania wa kutovaa barakoa na badala yake akavalia kifaa hicho kipindi chote cha ziara yake.

    Wakati wa hotuba yake , akiitoa kwa lugha ya Kiswahili ambayo raia wa mataifa hayo mawili hutumia kuwasiliana , aliwafurahisha viongozi wa kibiashara na wabunge kwa misemo .

    Hizi hapa ni baadhi ya nukuu tano bora za matamshi yake:

    'Mbuzi na barakoa'

    Rais huyo mwenye umri wa miaka 61 alitambua ziara yake ilikuwa inafanyika wakati mgumu sana wakati ambapo tunakabiliwa na mlipuko wa virusi vya corona.

    ''Tuko hapa kila mtu na barakoa usoni - na ninapowaona watu wamevalia barakoa inanikumbusha kijijini mwetu, wakati tulipokuwa tukienda kulisha mifugo, tunawafunga mbuzi kitu mdomoni ili kuwazuia kula mimea ya watu tukielekea malishoni sawa na tunavyofanya leo…lakini lazima tufanye."

    Tunaunganishwa na wanyamapori

    Ili kusisitiza kuhusu umuhimu wa biashara kati ya nchi majirani wa Afrika mashariki, inayoleta $450m (£324m) kwa mwaka , alitumia mfano wa Wild beest wanaovuka kutoka hifadhi ya wanyama pori ya Masai Mara na kuelekea Hifadhi ya wanyamapori ya Serengeti nchini Tanzania ili kuwasilisha ujumbe:

    "Mungu amezibariki nchi hizi mbili kuwa majirani. Tuna mipaka ya ardhi na majini. Na hata mazingira yetu yanafanana. Hata Wanyama wetu ni familia na majirani.

    Kuna hawa Wanyama wanaitwa Wildbeests , ambao huja kupata ujauzito nchini Kenya na kujifungua nchini Tanzania , sasa iwapo Wanyama wangekuwa na uraia wangekuwa raia wa taifa gani?"

    Wakenya wanavyong'ang'ana kuzungumza Kiswahili.

    Watanzania , hususan wale kutoka Zanzibar kama Rais Samia hupendelea kuzungumza kile kinachoitwa Kiswahili sanifu .

    Kiswahili cha Kenya upande mwengine ni kile cha kawaida - kikidaiwa na wengine kuwa kibaya na ndio chanzo cha uchokozi kati ya majirani hao wawili.

    "Tunafurahia uamuzi wenu kuanza kutumia lugha ya Kiswahili katika bunge. Hiyo ndio sababu inayonifanya mimi Kusikiliza vikao vya bunge vya Kenya - napenda Kiswahili chenu. Kiswahili chenu kina changamoto . changamoto hizo pekee zinaburudisha.

    ''Nilikuwa nikimsikiliza Spika akishindwa kutaja nambari za mwaka kwa Kiswahili''.

    Matumizi ya majina ya marais wote wawili

    Alifanya mzaha na jina lake na lile la mwenzake Uhuru Kenyatta ili kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya nchi hizo mbili.

    "Tuna bahati kwamba kati ya majina yetu kuna Uhuru wa kufanya biashara na suluhu ya kuondoa vikwazo vya kibiashara , Jukumu sasa ni lenu nyinyi. "

    Mvuto wa jiji la Nairobi

    Bi Samia alizungumzia kuhusu maisha ya Nairobi na raha yake ambayo imeathiriwa na masharti ya virusi vya corona .

    ''Nimegundua kuwa idadi kubwa ya ujumbe niliokuja nao wanajua vichochoro vya Nairobi, wanajua pale ambapo wanaweza kupata 'nyama choma' ''.

    "Lakini kwasababu ya corona hawawezi kufurahia , nina wasiwasi kwamba baadhi yao huenda wakasalia nyuma."


    RADIO JAMBO FREQUENCIES

    Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


    logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved