Muturi atawazwa kuwa msemaji wa Mlima Kenya licha ya pingamizi

Image: the-star

Spika  wa bunge la kitaifa Justin Muturi hatimaye jana alitawazwa kuwa msemaji wa eneo la Mlima Kenya katika hafla maalum iliyofanyika kwenye hekalu ya Mukurwe wa Nyagathanga licha ya pingamizi kali kutoka kwa wazee na viongozi mbali mbali.

Muturi  alitawazwa katika hafla iliyokuwa chini ya ulinzi mkali ambapo zaidi ya wazee elfu 1 kutoka kaunti mbali mbali walikusanyika hekaluni. Gavana wa Murang’a Mwangi wa Iria sasa anasema ataandaa hafla ya kutakasa hekalu hiyo kufuatia uteuzi wake Muturi.

Hayo yakijiri, naibu Rais  William Ruto jana alifanya mkutano na kikao cha kujadili uchumi wa eneo la pwani uliowaleta pamoja viongozi kutoka kaunti sita katika ukanda huo.

Kikao hicho kilifanyika katika kaunti ya Kilifi ambapo Ruto alionekana kuvumbua mkondo tofauti kabisa wa kuwavutia wapiga kura katika agenda yake ya Urais mwaka 2022.

Mbali na siasa, polisi huko Meru wamekamata watu 31 kutoka Ethiopia na Eritrea kwa kuwa humu nchini kinyume cha sheria.

Watu hao walipatikana wamejificha katika shamba moja la miraa huko Igende. Afisa wa DCI wa eneo hilo Calvin Ambaga anasema washukiwa hao watafikishwa mahakamani kesho.

Kwingineko, waziri wa usalama  Fred Matiang'i amewaagiza makamishna wa kaunti kuhakikisha kwamba machifu wa maeneo wanayosimamia wanaanzisha miradi ya kupanda miti. Anasema huku kutasaidia serikali kuafikia asilimia kumi ya misitu nchini  kufikia mwaka ujao.