BARABARA YA ATWOLI

Barabara ya Atwoli yaibua gumzo kubwa mitandaoni

Kaunti ya Nairobi inayoongozwa na Ann Kananu ilibadilisha jina la iliyokuwa 'Dik Dik Road' na kuipa jina mpya 'Francis Atwoli Road'

Muhtasari

Wakenya wengi mitandaoni wameonyesha kutoridhishwa kwao na hatua ya serikali ya Kaunti ya Nairobi kupatia barabara jina lake katibu mkuu wa COTU.

Francis Atwoli Road
Francis Atwoli Road
Image: Twitter

Wakenya mitandaoni wameonyesha kutoridhishwa kwao na hatua ya serikali ya Kaunti ya Nairobi kupatia barabara jina lake katibu mkuu wa COTU, Francis Atwoli.

Kaunti ya Nairobi inayoongozwa na Ann Kananu ilibadilisha jina la barabara ya 'Dik Dik Road' iliyoko katika maeneo ya  Kileleshwana, Nairobi na kuipa jina mpya 'Francis Atwoli Road'

Huku akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa barabara hiyo, Atwoli alisema kuwa hicho ni kitendo cha heshima sio kwake tu bali pia viongozi wengine wa muungano wa wafanyikazi nchini ambao walioaga.

"Ningependa kushukuru uongozi wa kaunti ya Nairobi chini ya Bi Ann Kananu kwa heshima hii na kwa kwa kutambua kazi ya serikali ya leo, jumuiya na wafanyakazi wote. Tutaendelea kushirikiana na uongozi wa kaunti hii" Atwoli aliandika kwenye mtandao wa Twitter.

Hata hivyo, jambo hilo lilionekana kuibua gumzo kubwa mtandaoni huku Wakenya wengi wakionyesha kughadhabishwa na kitendo hicho. Wengi waliachilia jumbe za kukashifu serikali ya Nairobi chini ya ujumbe wa Atoli akipongeza kaunti hiyo huku wengine wakiandika jumbe zao kando.

"Barabara ya Francis Atwoli ni tusi kubwa sana kwa Wakenya" Robert Alai aliandika.

"Ati gavana Ann Kananu amemtunuku Atwoli? Wananchi hawakuhusishwa, naenda kotini, hii haiambatani na sheria, itupiliwe mbali" mtumizi mwingine wa Twitter @kennethnmwiti alisema.

"Amefanyia Wakenya nini haswa? Hakuna chochote cha kuzungumzia baada ya miaka hiyo yote! " @x_stopher aliandika.

Hata hivyo, Wakenya wengine walimpongeza kiongozi huyo ambaye ameongoza COTU kwa kipindi cha miaka ishirini sasa wakisema kuwa alistahili heshima ile.

"Ni muhimu kupongeza Wakenya mashuhuri wakati ambao bado wako hai. Huwa tunangoja miaka baada wametuacha kujifanya vile tuliwapenda. Hongera, Bw Atwoli, umeheshimika vilivyo" @ItsMutai aliandika

"Wakenya wengine waweza kuwa na maoni tofauti lakini Bw Atwoli amefanya COTU kutambulikana nchini. Miungano ya wafanyakazi sio ya watu wenye roho nyepesi, Hongera" @Dr_Mndonye alichapisha.

Hizi hapa baadhi ya hisia za Wakenya katika mtandao wa Twitter.

 

Je, hisia zako ni zipi kuhusiana na uzinduzi wa Barabara ya Atwoli?