HONGERA NAKURU

Nchi ya Kenya kupata jiji la nne

Rais Kenyatta atarajiwa kukabidhi mji wa Nakuru hati ya kuwa jiji baada ya maseneta kupitisha pendekezo la kuinua hadhi ya mji huo.

Muhtasari

•Nakuru itakuwa inaungana na Nairobi, Mombasa na Kisumu kwenye orodha ya jiji za Kenya.

mji wa nakuru
mji wa nakuru
Image: Twitter

Huenda mji wa Nakuru ukatangazwa kuwa  jiji hivi karibuni baada ya maseneta kupitisha hoja ya kuinua hadhi ya mji huo ulio katika eneo la bonde la ufa.

Kamati ya ugatuzi ikiongozwa na seneta wa Homabay, Moses Kajwang' ilipendekeza kuinuliwa kwa hadhi ya Nakuru na kuwasilisha ripoti kwenye seneti siku ya Alhamisi.

Kamati hiyo ilionelea kuwa mji huo ulikuwa umeafikia umehitimu kufanywa mji jambo ambalo lilithibitishwa na maseneta wengine.

Lililobaki sasa ni rais Uhuru Kenyatta kuukabidhi mji huo hati ya kuthibitisha hali hiyo.Serikali ya kaunti ya Nakuru iliwasilisha ombi la kufanya Nakuru mji mwezi wa Novemba mwakani 2020. Kufuatana na hayo, kamati ya ugatuzi imekuwa na vikao 11 kuhadiliana kuhusu ombi hilo.

Baada ya vikao hivyo, kamati ya ugatuzi ilithibitisha kuwa mji wa Nakuru ulikuwa umefikisha matakwa ya kufanywa mji katika maswala ya idadi ya watu na mapato.

Kwa sasa mji wa Nakuru una zaidi ya watu 350,000, juu ya idadi ya 250,000 inayohitajika kufanywa jiji.

 

Seneta wa Elgeyo Marakwet, Kipchumba Murkomen alisihi serikali ya kaunti ya Nakuru kuwekeza katika kukuza miundombinu ya mji huo.

"Ni sharti serikali ya kaunti ya Nakuru iwe na idara maalum ya mipango na ujumbe wazi kwa wawekezaji wanaotaka kujenga jijini Nakuru kuwa lazima waje na ubunifu wa kipekee kwa mfano jumba lililo na mchoro wa flamingo unaweza vutia watalii sana" Murkomen alisema kwenye seneti.

Gavana wa kaunti hiyo ameshukuru Mungu kwa kupitisha ombi hilo kupitia mtandao wa Twitter.

Nakuru itakuwa inaungana na Nairobi, Mombasa na Kisumu kwenye orodha ya jiji za Kenya.