SIASA ZA 2022

Mutua ashauri rais Kenyatta, Raila na Kalonzo kukoma kutusi Ruto

Gavana huyo amesema kuwa maneno makali yanayoelekezewa naibu rais ili kumdhalilisha badala yake yanampa umaarufu wa kisiasa.

Muhtasari

•Gavana Mutua na ambaye ni kiongozi wa chama cha Maendeleo Chap Chap amekuwa kwenye ziara ya siku nne kwenye eneo la Mt Kenya na kukutana na magavana  pamoja na wanachi wa maeneo hayo.

•Kinara wa ODM Raila Odinga ameendelea kusisitiza kuwa bado hajatangaza kama atawania kiti hicho ama ataunga mkono mtu mwingine.

Gavana Alfred Mutua akihutubia wakazi wa Machakos
Gavana Alfred Mutua akihutubia wakazi wa Machakos
Image: Hisani

Gavana wa Machakos Alfred Mutua ameshauri viongozi wakubwa nchini kukoma kujadili naibu rais William Ruto kila wanapopata nafasi ya kuhutubia Wakenya.

Kulingana na Mutua,maneno makali ambayo viongozi wakubwa wanaelekezea naibu rais kila uchao ili kumdhalilisha, badala yake yanasaidia kumpaa umaarufu mkubwa kwa wananchi.

Kupitia ujumbe ambao alitoa siku ya Alhamisi, Mutua amewataka rais Uhuru Kenyatta, kinara wa ODM Raila Odinga, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na viongozi wengine wakuu kushirikiana  na wadau wengine kwenye ulingo wa siasa kutafuta njia za kutatua shida zinazowakumba Wakenya.

"Nchi yetu inakumbwa na shida nyingi ambazo zinahitaji kushughulikiwa na viongozi wa kisiasa wakuu nchini kama vile rais Uhuru Kenyatta na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga kushirikisha washika dau wengine kama mimi na viongozi wa vyama vingine ili kupata suluhu ya shida hizo" Mutua alisema.

"Maoni yangu ni kuwa malumbano ya kisiasa ,udhalilishaji na kelele zinazoelekezewa naibu rais zinasaidia tu kumjengea jina na kumpa umaarufu wa kisiasa" Mutua aliendelea kusema.

Amesema kuwa maoni hayo sio yake binafsi tu  ila amepokea maoni kama hayo kutoka kwa wananchi ambao amekuwa akikutana nao kwenye ziara yake ya kutangaza nia yake ya kuwania urais katika eneo la mlima Kenya.

"Nimeketi na kuskiza wananchi wakizungumzia mambo yaliyo karibu na nyoyo zao na wanavyotaka kukombolewa kutoka kwenye shida za kiuchumi" alieleza gavana Mutua.

Gavana Mutua na ambaye ni kiongozi wa chama cha Maendeleo Chap Chap amekuwa kwenye ziara ya siku nne kwenye eneo la Mt Kenya na kukutana na magavana  pamoja na wanachi wa maeneo hayo.

Kati ya kaunti alizozuru ni pamoja na Kirinyaga, Nyeri, Embu, Kiambu na Murang'a. 

Siku ya Alhamisi aliabiri garimoshi na kuzuru maeneo ya Embakasi ambako alikutana na wananchi. 

Mutua ni baadhi ya wanasiasa ambao wametangaza nia yao ya kuwania kiti cha urais. Wengine ambao wametangaza ni pamoja na  William Ruto, Mukhisa Kituyi, Musalia Mudavadi na Kalonzo Musyoka.

Kinara wa ODM Raila Odinga ameendelea kusisitiza kuwa bado hajatangaza kama atawania kiti hicho ama ataunga mkono mtu mwingine.